1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

New Zealand yaomboleza mashambulizi ya Christchurch

Admin.WagnerD22 Machi 2019

New Zealand inakumbuka leo  watu 50 waliouwawa kwenye shambulio la kigaidi. Pia katika mkutano wa Jumuiya ya nchi za kiislam unaoendelea nchini Uturuki, mashambulizi hayo yamekua pia ni dhima kubwa.

https://p.dw.com/p/3FUKV
Neuseeland Freitagsgebet in Christchurch nach Anschlägen auf zwei Moscheen
Picha: picture-alliance/AP Photo/V. Thian

Waislam nchini New Zealand wameitisha sala ya Ijumaa ambayo imetangazwa na vyombo vya habari mbalimbali katika nchi nzima. Maelfu ya watu wameshiriki katika sala hiyo ya kuwakumbuka watu 50 waliouliwa kwa kupigwa risasi wakiwa miskitini Ijumaa iliyopita.

Waziri mkuu wa New Zealand Jacinta Ardern pia alikuwa miongoni mwa watu  elfu 20 waliokua wamesimama katika bustani ya Hagley mbele ya msikiti wa Al Noor ambapo watu  wengi wa wahanga waliuliwa.

Bi Ardern amewaambia Waislamu wa New Zealand kwamba taifa zima linalia pamoja nao, na umati huo ulisimama kimya kwa kwa dakika mbili kwa ajili ya kukumbuka watu hao waliouliwa.

Waziri huyo wa New Zealand aliyepinga vikali mauaji hayo na kuyaita ni ya kigaidi, jana alitangaza  marufuku dhidi ya silaha za kivita kama zilizotumika na muuaji huyo Ijumaa iliyopita.

Hisia bado ni kali

Türkei Istanbul Besuch Außenminister Neuseeland Winston Peters
Kikao cha jumuiya ya ya nchi za kiislam ambacho waziri wa mambo ya nje wa New Zealand, Winston Peters ameshiriki.Picha: picture-alliance/AA/E. Yorulmaz

Huku sala hiyo ikiendelea, mkutano wa Jumuiya wa nchi za kiislam umeanza leo nchini Uturuki katika jiji la Instanbul ukigubikwa pia na tukio hilo la kigaidi dhidi ya miskiti nchini New Zealand.

Katika mkutano huo Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan alimpongeza Waziri mkuu wa New Zealand jinsi alivyoshughulika na mashambulizi hayo.

Pia  Erdogan alishukuru  vyombo vya usalama vya New Zealand kwa kuhakikisha wanafanya jitihada dhidi ya mauaji kama hayo.

Waziri wa mambo ya nje wa New Zealand, Winston Peters, aliyefika Uturuki leo asubuhi aliuambia mkutano huo wa Jumuiya ya nchi za kiislamu kwamba New Zealand itaendelea kuhakikisha Waislam wote wanaoishi katika nchi hiyo wataendelea kuishi kwa amani na bila wasiwasi licha ya hayo mashambulizi yaliyotokea.

Mwandishi: Harrison Mwilima/RTRE1/AFPE

Mhariri: Daniel Gakuba