1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK: Nchi za magharibi zakaribisha vikwazo vya kimataifa dhidi ya Korea kaskazini

16 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD2R

Nchi za magharibi zimekaribisha hatua ya Umoja wa mataifa ya kuiwekea vikwazo Korea ya kaskazini kufuatia jaribio lake la kuripua bomu la kinyuklia hivi karibuni. Balozi wa Uingereza kwenye Umoja wa mataifa, Emyr Jones Parry, amesema vikwazo vinailenga serikali na wala sio raia. Azimio la Umoja wa mataifa na ambalo lilipitishwa kwa kauli moja na wajumbe wa Baraza la usalama la Umoja wa mataifa, linaiwekea Korea ya kaskazini vikwazo vya silaha. Nilaruhusu pia kupekuliwa meli zinazotoka au zinazoelekea katika nchi hiyo, kuzuwia fedha zilizoko nje na kukataza biashara ya bidhaa zisizokuwa muhimu.

Lakini tayari Uchina imesema kupekuliwa kila meli inayokwenda au inayotoka Korea ya kaskazini ni jambo lisilokubalika. Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, bibi Condoleeza Rice, anatarajia kufanya ziara nchini Uchina, Japani na Korea ya kusini mnamo wiki hii kutafuta uungwaji mkono zaidi kwa azimio hilo.