1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK: Israel iko tayari kushirikiana na serikali mpya ya Palestina

18 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBqe

Israel imesisitiza kuwa iko tayari kushirikiana na serikali mpya ya mamlaka ya Palestina iliyopendekezwa na rais Mahmoud Abbas.

Akizungumza baada ya kufanya mazungumzo na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, alisema anatumai serikali mpya ya Wapalestina isiyojumulisha wajumbe wa kundi la Hamas, itakuwa mshirika wa maana katika juhudi za kutafuta amani ya Mashariki ya Kati.

Ehud Olmert aliashiria kwamba Israel iko tayari kulegeza sheria za usafiri katika eneo la ukingo wa magharibi wa mto Jordan na kutoa nusu ya kiwango cha dola milioni 700 za kimarekani inazoziulia kama ushuru wa serikali ya mamlaka ya Palestina.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ameikaribisha serikali mpya ya mpito ya mamlaka ya Palestina lakini wakati huo huo akaeleza wasiwasi wake juu ya machafuko yanayoendelea katika maeneo ya Wapalestina.

´Hali iliyozorota katika Ukanda wa Gaza na katika eneo zima la Mashariki ya Kati imekuwa shina la wasiwasi mkubwa miongoni mwetu. Na kushindwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa ya mamlaka ya Palestina ni kikwazo kikubwa kwa juhudi za kuboresha hali ya kibinadamu, usalama na kuendeleza mchakato wa kutafuta amani ya Mashariki ya Kati.´

Hii leo Israel imesema itatumia njia mpya za kuruhusu misaada ya kiutu kuingia Ukanda wa Gaza bila kushirikiana na chama cha Hamas.