1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

New York. Brown ahutubia kwa mara kwanza baraza kuu la umoja wa mataifa.

1 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBdG

Waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown amelihutubia baraza kuu la umoja wa mataifa mjini New York katika ziara yake ya kwanza katika umoja huo tangu kuingia madarakani.

Brown ametumia hotuba yake kutangaza mamlaka mapya ya umoja wa mataifa kwa ajili ya jimbo la Darfur.

Amesema kuwa hali katika jimbo la Darfur ni maafa makubwa ya kiutu, dunia inayokabiliana nayo hivi sasa. Watu laki mbili wameuwawa, milioni mbili wamekimbia makaazi yao na karibu milioni nne wanaishi kwa msaada wa chakula. Kufuatia mkutano jana na rais Bush, Uingereza na Ufaransa zimetoa azimio ambalo limeidhinishwa na baraza la usalama la umoja wa mataifa ili kutoa uwezo kwa jeshi kubwa kabisa la umoja huo kuwekwa katika jimbo la Darfur ili kulinda usalama wa watu wa jimbo hilo.

Uingereza na Ufaransa ni wadhamini wakuu wa azimio hilo, ambalo linatumia sura ya saba ya mkataba wa umoja wa mataifa, ambapo chini yake umoja wa mataifa unaweza kuidhinisha matumizi ya kijeshi.

Brown pia alilenga katika ukosefu wa hatua za maendeleo katika malengo manane ya maendeleo ya milenia yaliyotangazwa 2000.

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon ameisifu hotuba ya Brown na kuahidi kuongoza juhudi za kimataifa kuweza kufanikisha malengo hayo kwa mujibu wa mpango huo ifikapo mwaka 2015.