1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK : Bashir akataa tena kikosi cha Umoja wa Mataifa

10 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCKa

Rais Omar Hassan al Bashir wa Sudan amekataa kuukubali mpango wa muda wa Umoja wa Mataifa kuimarisha kikosi cha Umoja wa Afrika kilioko Dafur na ametowa wito wa kufanyika mazungumzo zaidi licha ya kukubali kimsingi katika makubaliano ya awali.

Akijibu baruwa kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ambayo shirika la habari la Uingereza Reuters imeipata hapo jana Bashir amesema bado haiko wazi iwapo Umoja wa Afrika ukikabiliwa na ukata wa fedha kwa kikosgi chake cha wanajeshi 7,000 huko Dafur utaendelea kudhibiti moja kwa moja shughuli hizo za kulinda amani.

Ameweka takriban hoja zake zote za kupinga mpango huo kwa kuzingatia vifungu vya Makubaliano ya Amani ya Dafur yaliofikiwa hapo mwezi wa Mei mwaka jana kati ya serikali na kundi moja la waasi ambapo amesema yanapingana na mipango ya Ban.

Baruwa hiyo iliokuwa ikitarajiwa kwa zaidi ya wiki sita zilizopita inavunja matumaini ya kuwekwa kwa wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa hivi karibuni huko Dafur ambapo takriban watu 200,000 wameuwawa, wengine milioni 4 wanahitaji misaada ya dharura na milioni mbili na nusu wanaishi kwenye makambi.