1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Obama: Amani idumishwe Mashariki ya Kati

Mjahida17 Oktoba 2015

Rais wa Marekani Barrack Obama ameelezea wasiwasi wake juu ya ghasia zilizoibuka mjini Jerusalem na kuwatolea mwito viongozi wa Israel na Palestina kuachana na maneno ya uchochezi.

https://p.dw.com/p/1Gpfs
Rais wa Marekani Barrack Obama
Rais wa Marekani Barrack ObamaPicha: Reuters/A. Kelly

Matamshi ya Obama yamekuja wakati kukiwa na ghasia kali kati ya maeneo ya Israel na Palestina zilizoleta hofu ya kuongezeka kwa machafuko. "Tunalaani matukio ya ghasia yanayoelekezwa kwa watu wasio na hatia na tunaamini kwamba Israel ina haki ya kudumisha utulivu na kuwalinda raia wake dhidi ya mashambulio ya kuchomwa visu pamoja na ghasia nyengine barabarani," alisema Barrack Obama.

Rais huyo wa Marekani aliongeza kuwa anaamini ni muhimu kwa Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, maafisa wengine wa Israel pamoja na kiongozi wa mamlaka ya wapalestina Mahmood Abbas, na watu wengine walio katika nafasi za uongozi kujaribu kujizuwiya na matamshi ya uchochezi yanayoweza kuzidisha ghasia, hasira, na kutoelewana.

Aidha mapigano makali yaliibuka hapo jana baada ya wapalestina kuchoma eneo la makaburi ya Joseph linaloheshimiwa na wayahudi mjini Nablus katika Ukingo wa Magharibi.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Kiongozi wa mamlaka ya Palestina Mahmood Abbas
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Kiongozi wa mamlaka ya Palestina Mahmood AbbasPicha: picture-alliance/dpa

Uchomaji huo ulitokea wakati wapalestina walipoitisha maandamano dhidi ya Israel na mapolisi waliowakataza kuhudhuria sala ya kila wiki katika msikiti wa Al Aqsa mjini Jerusalem.

Mpaka sasa Waisrael wapatao saba wameuwawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika ghasia hizo huku Wapalestina 37 wakiuwawa na wengine wengi kujeruhiwa katika machafuko hayo.

Kerry awaomba viongozi wa Israel na Plaestina kudumisha amani

Huku hayo yakiarifiwa Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry ambaye yuko Milan katika ziara yake barani Ulaya, alizungumza na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu siku ya Ijumaa kujadili namna ya kumaliza ghasia hizo na kutoa uungaji mkono wa Marekani katika upatikanaji wa mikakati ya kutuliza hali haraka iwezekanavyo.

Siku ya Alhamisi Kerry pia alizungumza na kiongozi wa mamlaka ya wapalestina Mahmood Abbas na kuhimiza umuhimu wa kujitenga na ghasia, maneno ya uchochezi, na hatua zinazoweza kuchochea machafuko zaidi.

Hata hivyo Netanyahu na Kerry wanatarajiwa kukutana mjini Berlin wiki Ijayo pamoja na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ili kujadili usalama wa eneo la Mashariki ya kati.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John KerryPicha: picture-alliance/AP Photo/E. Vucci

Kwengineko Palestina imelihimiza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutoa mara moja ulinzi wa Kimataifa kwa watu wa Palestina kufuatia mzozo unaoendelea kutanuka kati yake na Israel, Israel imekataa kuwepo kwa majeshi ya Kimataifa katika eneo takatifu la Jerusalem. Hatua ya majibizano iliokuwepo katika mkutano huo wa dharura wa Baraza hilo uliyoitishwa na mataifa ya Kiarabu imeonyesha hasira na kutoaminiana kati ya nchi hizo mbili Isarel na Palestina baada ya miongo kadhaa ya mgogoro.

Kwa upande wake Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa Riyad Mansour ameliambia baraza hilo hatua ya ulinzi inahitajika kwa sasa kuliko muda mwengine wowote ule, kwa sababu ya kile alichokiita uchokozi wa Israel dhidi ya watu wasioweza kujilinda wa Palestina.

Lakini Balozi mpya wa Israel katika Umoja wa Mataifa Danny Danon, amelihimiza baraza hilo kuvunja ukimywa wake na kutoa taarifa dhidi ya uchochezi unaosababisha hofu na vile vile kuunga mkono majadiliano ya moja kwa moja kati ya Israel na Palestina.

Balozi Danon amemshutumu Mahmood Abbas kwa kuongoza visa vya uchochezi kutokana na matamshi yake ya chuki na kudai kuwa Israel inajaribu kubadilisha hali iliopo katika eneo la Jerusalem

Mwandishi Amina Abubakar/AFP/AP/ Reuters

Mhariri: Sekione Kitojo