1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha Yisrael Beitenu kuungana na serikali yake

Sylvia Mwehozi25 Mei 2016

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akubaliana na chama cha kizalendo cha Yisrael Beitenu kuungana na serikali yake. Kiongozi wa chama hicho Avgdor Lieberman sasa atakuwa waziri wa Ulinzi .

https://p.dw.com/p/1Iu3s
Israel Benjamin Netanjahu Knesset in Jerusalem
Picha: picture-alliance/dpa/A. Sultan

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amefikia makubaliano na chama cha kizalendo kuungana na serikali yake.Katika makubaliano hayo chama cha Yisrael Beitenu kinachoongozwa na Avigdor Lieberman sasa kitaungana na Muungano unaounda serikali ya Netanyahu na kuongeza wabunge watano.

Lieberman ambaye amekuwa na kauli kali juu ya hatua dhidi ya wapalestina anaowaita"magaidi"anatarajiwa kuchukua nafasi ya waziri wa ulinzi.

Waziri wa utalii Yariv Levin ambaye ni msuluhishi kwa upande wa chama cha Netanyahu cha Likud ameiambia radio ya taifa kuwa makubaliano hayo tayari yamefikiwa wakati ambapo pia msemaji wa Lieberman naye akithibitisha kwa shirika la habari la AFP, makubalianao hayo yatasainiwa hapo baadae siku ya jumatano .

Hatua ya Lieberman mwenye umri wa miaka 57 ya kupatiwa wizara nyeti ya ulinzi, imezusha wasiwasi miongoni mwa wanasiasa wa mrengo wa kati na ule wa kushoto pamoja na wanasiasa katika chama cha Likud.

Viongozi wa dini wazalendo kutoka chama cha wayahudi tayari wanashikilia nafasi muhimu katika baraza la mawaziri la serikali ya Netanyahu.

Waziri wa ulinzi aliyejiuzulu hapo ijumaa Moshe Yaalon , mwanachama wa Likud na ambaye aliwahi pia kuwa mkuu wa majeshi alionya kwamba.

Waziri mkuu wa zamani na kutoka chama cha labour ambaye pia aliwahi kuwa waziri wa ulinzi Ehud Barak, amekwenda mbali na kusema serikali ya Israel "imeambukizwa ufashisti."

Wengine wanasema Lieberman katika wote wanaotaka kuwa waziri mkuu siku moja, atakabiliana na upinzani mkali hasa kuhusu suala la usalama kutokana na mawazo yake yaliyo na utata.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akifanya mazungumzo na Avigdor Lieberman
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akifanya mazungumzo na Avigdor LiebermanPicha: Reuters/A. Cohen

Mfano mzuri ni kauli yake ya kichokozi aliyoitoa hivi karibuni kwa kiongozi wa kiislamu wa harakati za Hamas katika ukanda wa Gaza , Ismail Haniya. Alimwambia Haniya kuwa angempatia saa 48 tu za kuwaachilia washikiliwa wawili wa Israel na miili ya askari waliouawa katika vita ya mwaka 2014 au"angekufa."

Makubaliano hayo yanahitimisha uvumi wa wiki kadhaa juu ya hatua ya Netanyahu ya kutaka kupanua serikali yake ambayo inashikilia viti 61 kati ya 120 katika bunge tangu uchaguzi wa machi 2015.

Awali Netanyahu alikuwa na mazungumzo na kiongozi wa chama cha labour, Isaac Herzog ili ajiunge na serikali yake kabla ya kumgeukia Lieberman.

Mbali ya Lieberman kuwa waziri wa ulinzi na mwenzake mwingine kuwa waziri wa uhamiaji, serikali pia imekubali kutenga kiasi cha dola milioni 363 kama pensheni kwa ajili ya wazee wa Israel.

Lieberman aliye mzaliwa wa jamhuri ya kisovieti ya Moldova anaweka mipango ya kuwasaidia wahamiaji kutoka taifa hilo la zamani la kisovieti ambako ndiko aliko na nguvu ya wapiga kura. Msemaji wake amesema kuwa"haya ndio mambo mawili makubwa katika jimbo letu la uchaguzi."

Alikuwa anaishinikiza serikali kuanzisha adhabu ya kifo kwa wapalestina anaowaita "magaidi"lakini hata hivyo aliyaondoa mahitaji hayo wakati wa mazungumzo.

Pamoja na makubaliano hayo, wachambuzi wanasema kuna uwezekano wa kubadilika kwa sera za sasa. Israel haijawahi tekeleza adhabu ya kifo tangu mwaka 1962.

Netanyahu katika kupunguza hofu ya uteuzi wa Lieberman , amesema kwamba ataendelea na mpango wa kutafuta amani na wapelestina pamoja na kusimamia sera za wizara ya ulinzi zinazotaka udhibiti wa ukingo wa magharibi.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP

Mhariri: Yusuf Saumu