Neil Armstrong afariki akiwa na umri wa miaka 82
26 Agosti 2012Alikuwa kamanda wa kikosi cha safari ya Apollo 11 - pamoja na mwanaanga mwengine Buzz Aldrin. Mamilioni ya watu duniani kote waliweza kufuatilia kwenye televisheni mnamo mwaka wa 1969, jinsi Armstrong alivyotua mwezini, umbali wa kilometa 400,000 kutoka kwenye sayari ya dunia.
Armstrong alisema wakati huo kwamba alichokifanya, ilikuwa ni hatua fupi kwake kama binadamu mmoja, lakini ilikuwa ni hatua ndefu mbele, kwa binadamu wote duniani. Rais Barack Obama amemsifu mwanaanga huyo kuwa ni shujaa mkubwa kabisa wa Marekani ambae kamwe hatasahaulika.
Armstrong aliefariki kutokana na matatizo yaliyoyababishwa na maradhi ya moyo, baada ya kuifanyiwa upasuaji mapema mwezi huu, amesifiwa kwa utayarifu wa kuzikabili na kuzishinda changamoto zilizoonekana kutoweza kushindika. Rais Obama aliyasema hayo wakati akiongoza katika kuwasilisha rambirambi pamoja na mwanaanga Buzz Aldrin. Obama amesema Armstrong alikuwa shujaa wa kweli.
Obama ameeleza kuwa wakati Armstrong na wanaanga wenzake walipoanza safari yao katika chombo cha Apollo 11 mnamo mwaka wa 1969, waliyabeba matumaini ya taifa lote la Marekani. Wakati huo Obama alikuwa bado ana wiki mbili ili kutimiza umri wa miaka minane. Obama amesema, alipotembea kwenye eneo la mwezini kwa mara ya kwanza ,Neil Amstrong alianzisha kipindi cha mafanikio ya mwanadamu ambacho kamwe hakitasahaulika.
Mwanaanga mwenzake, aliefuatana naye katika safari ya mwezini,Buzz Aldrin amesema ana uhakika kwamaba mamilioni ya watu wameungana naye katika kuomboleza kifo cha shujaa huyo wa Marekani. Buzz Aldrin amesema atamkumbuka rafiki yake Armstrong kama jinsi wananchi wengine wa Marekani na wote duniani watakavyomkumbuka mwanaanga huyo maarufu. Licha ya mafanikio yake makubwa yaliyotokana na safari ya Apollo11 Armstrong hakuwa mpenda sifa wa vyombo vya habari na wakati wote alijaribu kuviepuka.
Armstrong hakuhisi kujitoa hadharani na kuvitumia vyombo vya habari. Hayo ameyasema mwanaanga mwengine wa Marekani John Glenn aliekuwa Mmarekani wa kwanza kuizunguka sayari ya dunia. Wajerumani pia wametoa rambi rambi zao juu ya kifo cha mwanaanga huyo wa Marekani na wamesifu mafanikio yake.
Mkuu wa Shirika la utafiti wa anga la Ujerumani Profesa Johann-Dietrich Wörner ameliambia shirika la habari la dpa, kwamba Armstrong aliyawakilisha mafanikio ya maalfu ya wahandisi waliofanya kazi kuifanikisha safari ya chombo cha Apollo 11.
Profesa huyo amesema Armstrong alikuwa ishara kwa binadamu ya kuonyesha kwamba juhudi zao za kutafiti mambo mapya zitahifadhiwa daima bila ya kujali iwapo utafiti huo utakuwa na faida kifedha.Profesa Wörner amesema Arsmstrong ataacha urithi utakaokumbukwa daima duniani kote hata baada ya kifo chake.
Mwandishi: Abdu Mtullya/AFP
Mhariri: Bruce Amani