1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege za kivita za Saudia zashambulia Aden

13 Aprili 2015

Ndege za kivita za Saudi Arabia pamoja na washirika wake zimeshambulia kusini mwa Yemen, yakiwemo makaazi ya rais yanayodhibitiwa na waasi wa Kishia wa Houthi mjini Aden.

https://p.dw.com/p/1F6uv
Vifaru vya kijeshi vya Yemen vikiwa Aden
Vifaru vya kijeshi vya Yemen vikiwa AdenPicha: Getty Images

Duru za madaktari na wakaazi wa maeneo hayo, zimeeleza kuwa ndege hizo za kivita leo zimeshambulia makaazi ya Rais Abed-Rabbo Mansour Hadi, kwenye mji wa kusini wa Aden, sehemu aliyokuwa akijihifadhi kabla ya kukimbilia nchi jirani ya Saudi Arabia, baada ya kuanza kwa mashambulizi ya muungano wa mataifa tisa ya Kiarabu Machi 26. Ndege hizo zimeshambulia pia maeneo ya waasi wa Houthi na katika vizuizi vya kuingilia Aden.

Taarifa zinaeleza waasi wa Houthi na washirika wao katika vitengo vya kijeshi vinavyomtii rais wa zamani wa Yemen, Ali Abdullah Saleh, vimepambana na wafuasi wa Hadi katika maeneo kadhaa ya jirani kwa usiku kucha. Kwa mujibu wa taarifa hizo, raia wawili pamoja na wanajeshi watatu wanaomtii Rais Hadi wameuawa leo baada ya kupigwa risasi, mjini Aden.

Watu walioshuhudia wamesema mashambulizi mengine ya anga yamefanyika pia kwenye jimbo la kusini mwa Yemen, Shabwa. Watu wenye silaha katika jimbo hilo, waliidhibiti ngome ya kijeshi ya waasi wa Houthi katika mji wa pwani wa Al-Nashima. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon jana alisema kuwa waasi wa Houthi wanajaribu kuidhibiti Yemen kwa kutumia nguvu.

Waasi wa Houthi
Waasi wa HouthiPicha: picture-alliance/AP Photo

''Hili halikubaliki. Lakini pia nina wasiwasi sana kutokana na kusambaa kwa mapigano ya kijeshi ambapo wahanga wa kiraia wanaongezeka na muindombinu ya umma inazidi kuharibiwa. Mzozo wa ndani wa Yemen haupaswi kuruhusiwa usambae hadi ufike kuwa mgororo wa kikanda,'' alisema Ban.

Mzozo kati ya Iran na Saudia wapamba moto

Wakati huo huo, Iran imesitisha safari za ndege za mahujaji kwenda Saudi Arabia kutokana na tuhuma za unyanyasaji wa ngono. Iran imeishutumu Saudi Arabia baada ya maafisa wawili wa usalama wa nchi hiyo kuwanyanyasa kingono vijana wawili wa Iran katika uwanja wa ndege wa Jeddah.

Shirika la habari la wanafunzi wa Iran-ISNA, leo limemnukuu Waziri wa Utamaduni wa Iran, Ali Jannati akisema kuwa safari hizo zimesitishwa hadi hapo watuhumiwa hao watakaposhtakiwa na kuadhibiwa. Kiasi Wairan 500,000 kila mwaka wanaenda kuhiji kwenye miji mitakatifu ya Mecca na Medina.

Waziri wa Utamaduni wa Iran, Ali Jannati
Waziri wa Utamaduni wa Iran, Ali JannatiPicha: MEHR

Mzozo wa kidiplomasia kati ya Iran na Saudi Arabia unazidi kupamba moto kutokana na mashambulizi ya anga yanayofanywa na Saudi Arabia na washirika wake, dhidi ya waasi wa Houthi nchini Yemen.

Ama kwa upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif, leo ametoa wito wa kuanzishwa kwa serikali mpya ya Yemen na amependekeza Iran iwe mchangiaji mkubwa katika kusaidia kuwepo kwa kipindi cha mpito cha kisiasa, kauli ambayo huenda ikaikasirisha vibaya Saudi Arabia.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo: AFPE,APE,RTRE
Mhariri:Yusuf Saumu