1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege ya Marekani yaanguka Iraq

22 Agosti 2007

Wanajeshi 14 wauwawa kufuatia ajali hiyo inayodaiwa kusababishwa na matatizo ya kiufundi

https://p.dw.com/p/CB1p
Picha: AP

Jeshi la Marekani limetoa taarifa kwamba ndege hiyo ilianguka kufuatia matatizo ya kimitambo.

Wakati huo huo waziri mkuu wa Iraq Nuri al Maliki ameyapinga matamshi ya Marekani ya kuikosoa serikali yake.

Ndege aina ya Helikopta ya jeshi la Marekani ilianguka katika eneo la kaskazini mwa Iraq leo hii na kusababisha kuuwawa kwa wanajeshi 14 waliokuwemo ndani.

Tukio hilo ndilo baya kabisa kuwahi kushuhudiwa na wanajeshi wa Marekani tangu mwezi Januari mwaka 2005.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na jeshi hilo ishara za mwanzo zimeonyesha kuwa ndege hiyo ilianguka kutokana na matatizo ya kimitambo.

Jeshi la Marekani limeondoa uwezekano kwamba ndege hiyo ilitunguliwa na wapiganaji wa Iraq.

Hata hivyo mahala halisi ilipoangukia helikopta hiyo hapakujulikana mara moja.

Ajali hiyo imefikisha idadi ya wanajeshi wa Marekani waliouwawa Iraq kuwa 3,721 tangu nchi hiyo ilipovamia Iraq mwaka 2003.

Wakati hayo yakiarifiwa katika eneo hilohilo la kaskazini mwa Iraq kiasi cha watu 20 wameuwawa wakati mshambuliaji wa kujitoa muhanga alipoligongesha gari lake dhidi ya tanki ya mafuta hadi ndani ya geti la kituo cha polisi kwenye mji ulio tete wa Baiji kilomita 180 kutoka mjini Baghdad.

Watu wengine 50 walijeruhiwa kufuatia shambulio hilo.

Wakati huo huo waziri mkuu wa Iraq Nuri al Maliki akikamilisha ziara yake ya siku tatu huko Syria ameyapinga matamshi ya kuikosoa serikali yake yaliyotolewa na Marekani na kusema kuwa ni wairaqi wenyewe watakaoamua hatma ya nchi yao na wala sio mtu mwingine.

Bwana Maliki amekuwa akizidi kukabiliwa na shinikizo kutoka Marekani juu ya kushindwa kwa serikali yake kupiga hatua katika suala la maridhiano baina ya wasunni na washia pamoja na kupitisha sheria zitakazounga mkono maridhiano hayo.

Hata hivyo waziri mkuu huyo wa Iraq amewaambia waandishi wa habari kwamba hakuna mtu yoyote aliyenajukumu la kuiwekea mipango serikali ya Iraq.Aidha amewashutumu wanasiasa wa Marekani na viongozi wa nchi hiyo kwa kutoa matamshi yasiyostahili pamoja na yakuikosoa serikali yake.

Kwingineko rais wa Iraq Jalal Talabani amepinga pendekezo la Ufaransa la kutaka kupatanisha makundi hasimu nchini Iraq akisema angependelea zaidi uwekezaji wa Ufaransa katika mafuta na kuijenga upya nchi hiyo.

Matamshi hayo ya Talabani yamekuja wakati waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Bernard Kouchner akifanya ziara ya ghafla mjini Baghdad yenye lengo la kuisogeza Ufaransa karibu na Iraq na kujenga urafiki na serikali ya mjini Washington ambao ulikuwa unayumbayumba kufuatia rais wa Zamani wa Ufaransa Jacque Chirac kupinga vikali vita vya Iraq vilivyoongozwa na Marekani