1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege iliyouwa wachezaji wa Chapecoense iliishiwa mafuta

1 Desemba 2016

Mawasiliano yaliyorekodiwa kutoka ndege iliyopata ajali nchini Colombia yanaeleza kuwa rubani wa ndege hiyo iliyokuwa imebeba wachezaji wa timu ya nchini Brazil ilikuwa imeishiwa mafuta muda mfupi kabla ya kuangua.

https://p.dw.com/p/2TZ3S
Kolumbien Absturzstelle des LaMia Flugzeugs
Picha: Reuters/F. Builes

Hayo ni  kwa mujibu wa kifaa cha kunasia mazungumzo hayo, ajali hiyo iliyotokea katika milima ya karibu na mji wa Medellin na kuuwa abiria 77. Maelezo ya mwisho kuhusu ajali hiyo yametolewa jana jumatano wakati ambapo mashabiki wa timu ya Chapecoence wakiendelea kuomboleza vifo vya wachezaji waliokuwa katika ndege hiyo. Abiria sita tu ndio walionusurika. Wengi wa waliopoteza maisha ni wachezaji wa klabu hiyo ya kandanda ambayo ilikuwa imeanza kupata umaarufu.

Katika maelezo ya kifaa kilichorekodi sauti zilizonukuliwa na vyombo vya habari vya nchini Colombia, yanaonyesha kuwa rubani wa ndege ya shirika la ndege la LAMIA, aliwasiliana na kitengo cha mawasiliano ya kuogoza ndege siku ya jumatatu usiku akiomba kibali cha kutua kwa dharura kwa sababu ya tatizo la mafuta. Muongozaji amethibitisha kupokea ombi hilo lakini alimwambia rubani huyo  Miguel Quiroga kuwa anatakiwa kusubiri kwa dakika saba ili aweze kutua.

"tuna tatizo la mafuta, ni dharura, ndio maana ninakuomba kwa ajili ya hilo mara moja tu basi, alisema rubani huyo.

Mtiririko wa matukio haukufahamika vizuri mara moja lakini baadae rubani aliwasiliana tena,baada ya muda mfupi mawasiliano yalikatika wakati rubani akiendele akiomba ruhusa ya kutua kwa dharura.

Kolumbien Tribut an die Chapecoense Fussballmanschaft
Mashabiki wa timu ya Chapecoense wakiomboleza.Picha: picture alliance/dpa/M. D. Castaneda

Shirika la safari za anga la Colombia limesema kuwa mawasiliano yaliyorekodiwa yalikuwa na mapungufu na halikutaka kuzungumza chochote kuhusiana nayo, japo mkuu wa kitengo cha usalama wa shirika hilo Freddy Bonilla alithibitisha katika mkutano wake na waandishi wa habari kuwa ni kweli ndege hiyo ilikuwa imeishiwa mafuta wakati ilipoanguka.

Bonila aliongeza kuwa sheria za kimataifa zinazitaka ndege kuwa na hifadhi ya mafuta wakati zikiruka kutoka uwanja mmoja kwenda mwingine na kuwa ndege ya shirika la LAMIA haikufanya hivyo.

Kisanduku cheusi cha kunasa mawasiliano ya rubani kimepatikana kikiwa katika hali nzuri, mamlaka zinasema kuwa wachunguzi kutoka Uingereza na Brazil wameelekea Colombia kusaidia uchunguzi

Mwandishi: Celina Mwakabwale/AFP

Mhariri:Gakuba Daniel