1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za G7 zinaanda lengo dhidi ya ugaidi

Admin.WagnerD8 Juni 2015

Viongozi wa dunia katika mkutano wa kilele wa nchi saba zilizowendelea kiviwanda ,kundi linalojulikana kama G7 leo wanaandaa lengo la pamoja kuanzia mapambano na vitisho vya ugaidi kutoka kwa wapiganaji wa Jihadi.

https://p.dw.com/p/1FdHU
G7 Runder Tisch Angela Merkel Barack Obama Francois Hollande
Viongozi wa G7, Angela Merkel Barack Obama na Francois HollandePicha: Reuters/M. Rehle

Hatua hiyo imetiliwa mkazo vilevile kutokana na kile kilicholaaniwa na Rais Barack Obama wa Marekani kuwa ni,” uchokozi wa Urusi nchini Ukraine.” Mkutano huo ulioanza jana katika mji wa Elmau kusini mwa hapa Ujerumani, haumshirikishi Rais wa Urusi Vladimir Putin ,ikiwa ni mara ya tatu.

Viongozi wa kundi hilo la nchi saba zilizoendelea kiviwanda G7,wamewaalika viongozi wengine nje ya kundi hilo, wakiwemo Waziri mkuu wa Iraq Haider al-Abadi na Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari, ambao wote wawili wanapambana na makundi ya itikadi kali ya Kiislamu katika nchi zao-Kundi linalojiita dola la Kiislamu-IS huko Iraq na Boko haram nchini Nigeria.

Sauti ya Iraq kusikika

Waziri mkuu Abadi anatarajiwa kuzungumzia kampeni inayoongozwa na marekani kuisaidia nchi yake kuyakomboa maeneo yanayoshikiliwa na wapiganaji hao wa IS, ambalo limetangaza Dola la Kiislamu nchini humo na katika nchi jirani ya Syria ambako pia inayadhibiti maeneo kadhaa.

Irak Ramadi Angriff IS
Mapigano dhidi ya IS nchini IraqPicha: picture-alliance/AP Photo

Kwa upande wake Rais Buhari wa Nigeria aliyeshika madaraka Mei 29, baada ya kumshinda Rais Goodluck Jonathan katika uchaguzi wa kidemokrasi, anatarajiwa kuwasilisha orodha ya msaada kwa viongozi hao kupambana na kundi la Boko haram linalolaumiwa kwa mauaji ya watu 15,000 tangu 2009.

Hapo jana siku ya kwanza ya mkutano wao, suala lililotawala lilikuwa ni mzozo wa Ukraine, huku Rais Obama wa Marekani na mwenyeji wa mkutano huo kansela wa Ujerumani Angela Merkel wakiitaka jamii ya kimataifa kusimama kidete dhidi ya Urusi hadi imeheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Ukraine yaliofikiwa katika mji mkuu wa Belarus-Minsk.

Wasiwasi wa Urusi

Ingawa Rais wa Urusi Vladimir Putin amesisitiza kwamba hakuna haja ya kuihofia Urusi, kupamba moto karibuni kwa mapigano kunatia wasiwasi kwamba makubaliano ya kusimamisha mapigano yaliofikiwa kutokana na juhudi kubwa za Ufaransa na Ujerumani miezi mine iliopita yanaweza kuvunjika.

Merkel aliiambia stesheni ya matangazo ya televisheni ya ZDF kwamba , tunapaswa kutuma ujumbe mkali hapa na kuwa na vikwazo vitakavyofikia malengo .

Suala jengine katika mkutano huo wa G7, ni mvutano baina ya Ugiriki na wakopeshaji wake wa kimataifa-Umoja wa Ulaya, Benki kuu ya Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa,IMF- na hofu ya kwamba kufilisika kwa nchi hiyo kutaisababisha kujiondoa katika kundi la nchi zinazotumia sarafu ya euro , wakati athari zake kwa uchumi wa dunia zikiwa hazijulikani zitakuwaje.

Wakati huo huo, Kansela Merkel na Rais Francois Hollande wa Ufaransa wanatarajiwa kupigania kupatikane maridhiano ndani ya kundi hilo la G7 kuhusu suala jengine zito la kimataiaf-mabadiliko ya tabia nchi- kabla ya mkutano wa kilele wa Umoja wa mataifa mjini Paris mwezi Desemba.

Mwandishi:Mohammed Abdul-Rahman, afp

Mhariri:Yusuf Saumu