1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za EU kuendelea na mkataba wa Iran

Grace Kabogo
7 Mei 2018

Ufaransa na Ujerumani zimesema zitaendelea kuuheshimu mkataba wa nyuklia wa Iran, bila kujali uamuzi utakaotolewa hivi karibuni na Marekani kuhusu kujiondoa au kuendelea na mkataba huo.

https://p.dw.com/p/2xJoF
Deutschland Maas und Le Drian dringen auf Erhalt des Atomabkommens mit Iran
Picha: imago/Jens Schicke

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas amesema haoni sababu ya kujiondoa kwenye mkataba huo uliosainiwa mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani, na wanataka kuendelea kuuheshimu. Maas ameitoa kauli hiyo leo mjini Berlin katika mkutano wa pamoja na waziri mwenzake wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian anayeizuru Ujerumani.

''Kwetu sisi ni wazi kwamba mkataba huu unaifanya dunia kuwa sehemu salama na bila ya mkataba huu dunia haitokuwa salama,'' alisema Maas.

Kwa wiki kadhaa Ufaransa, Ujerumani na Uingereza zimekuwa zikiendesha kampeni ya kuendelea na mkataba huo na tangu mwezi Januari wamekuwa wakijadiliana na Marekani kutafuta njia za kumshawishi Rais Donald Trump kutouvunja mkataba huo. Maas amebainisha kuwa kuna mapendekezo kadhaa yamewasilishwa katika wiki za hivi karibuni.

USA Präsident Donald Trump zurück im Weißen Haus nach NRA Forum NEU
Rais wa Marekani, Donald TrumpPicha: picture-alliance/Pacific Press/M. Candelori

Trump ametishia kujiondoa kwenye mkataba wa nyuklia kwa kuvirejesha vikwazo kwa Iran pindi vitakapomalizika muda wake tarehe 12 ya mwezi huu wa Mei, hadi hapo nchi za Ulaya zilizosaini makubaliano hayo zitakaporekebisha kile alichokiita ''kasoro'' zilizoko katika baadhi ya vipengele.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian amesema hawaoni kama kuna sababu yoyote ya kujiondoa kwenye mkataba huo na wataendelea kuwashawishi hivyo marafiki zao wa Marekani.

''Tumeamua kuendelea na mkataba wa nyuklia kwa sababu ni njia sahihi ya kuizuia Iran kutengeneza na kutokuwa na silaha za nyuklia. Mkataba huu unahitaji kudumishwa na tutauendeleza licha ya uamuzi utakaochukuliwa na Marekani,'' alifafanua Le Drian.

Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Boris Johnson amemsihi Trump kutojiondoa kwenye mkataba wa Iran, akisema kwamba wakati Trump ana haki ya kuzungumzia kasoro zilizopo katika makubaliano hayo, jumuia ya kimataifa haikuwa na njia nyingine mbadala ambayo ni bora zaidi.

Iran Hassan Rouhani
Rais wa Iran, Hassan RouhaniPicha: picture alliance/AP Photo/Iranian Presidency Office

Katika juhudi za kuifanya Marekani iendelee na mkataba huo, nchi hizo tatu za Umoja wa Ulaya zimekuwa zikijadiliana jinsi ya kupambana na mpango wa makombora wa Iran, shughuli za kinyuklia za Iran baada ya mwaka 2025 wakati masharti muhimu ya mkataba yatakapokamilika pamoja na jukumu lake katika vita vya Syria na Yemen.

Wakati huo huo, Rais wa Iran, Hassan Rouhani amesema nchi yake haiko tayari kuachana na mpango huo wa nyuklia hata kama Marekani itajiondoa. Rouhani amesema kama Marekani itajiondoa itakuwa imefanya kosa kubwa sana na itaujutia uamuzi wowote ule wa kuachana na mpango wa nyuklia. Amebainisha kuwa Iran itapinga kwa nguvu zote shinikizo la Marekani kuizuia na kudhibiti ushawishi wake katika Mashariki ya Kati.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, AFP, Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman