1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO na Urusi uso kwa uso

4 Julai 2011

Wawakilishi wa Jumuia ya Kujihami ya NATO na Urusi wanakutana hii leo katika mjini Sotschi nchini Urusi kuzungumzia, pamoja na mengine, uwezekano wa kuunda mfumo wa pamoja wa kinga dhidi ya makombora kutoka maadui zao.

https://p.dw.com/p/11oiy
Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen
Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh RasmussenPicha: AP

Pengine hali nzuri ya hewa katika mji huo wa mwambao wa Bahari Nyeusi itasaidia kidogo kutuliza nyoyo za wanaohudhuria mkutano huo.

Rais Dmitry Medvedev wa Urusi na Katibu Mkuu NATO, Anders Fogh Rasmussen, watashiriki katika mkutano huo utakaowaleta pamoja wawakilishi wa kudumu wa pande hizo mbili.

Balozi wa Urusi kwenye Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Dmitri Rogosin, anasema ana uhakika kuwa mazungumzo kuhusu mfumo wa Ulaya wa kinga dhidi ya makombora yatakuwa makali.

"Wenzetu na marafiki zetu wa Marekani wanaujua vilivyo msimamo wa Urusi. Nchi za Ulaya zisijigeuze mashahidi tu. Kwa sababu kimsingi mtambo huo utategwa katika ardhi yao. Kwa hivyo, tuache mtindo wa kunyamaza na kujificha nyuma ya mbabe." Amesema Rogosin.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel (kulia) na Rais wa Urusi, Dmitry Medvedev
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel (kulia) na Rais wa Urusi, Dmitry MedvedevPicha: AP

Mjini Sotschi, Warusi wanataka wapatiwe msimamo bayana jinsi mfumo huo wa kinga dhidi ya makombora utakavyokuwa. Ingawa kimsingi paande zote mbili zinakubaliana kushirikiana katika mradi huo, lakini mvutano mkali unpo juu ya namna yenyewe ya kuundwa kwa mfumo huo.

NATO inataka kufuata mipango ya mtambo wa kinga ya makombora iliyoandaliwa na Marekani kwa ajili ya ardhi ya Ulaya na inashauri Warusi wabuni mtambo wao wenyewe wa kinga.

"Ndoto yetu ni kuwa na mifumo miwili ambayo ina lengo moja: watu wabadilishane habari na kuimarisha ulinzi wa maeneo ya NATO na yale ya Urusi." Alisema Rasmussen wakati wa mkutano kama huu wa NATO na Urusi mapema mwezi Juni 2011.

Na msimamo huo hautarajiwi kubadilika katika mazungumzo ya leo ya Sotschi.

Mwandishi: Nagel Christina (WDR)
Tafsiri: Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman