1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa kihistoria

Admin.WagnerD7 Januari 2015

Rais wa Sri Lanka Mahinda Rajapaksa anakabiliwa na changamoto isiyo kifani kutoka kwa upinzani uliojipanga upya, katika uchaguzi mkuu unaofanyika Alhamisi, miaka mitano baada ya kulishinda kundi la waasi wa Tamil.

https://p.dw.com/p/1EGCr
Sri Lanka - Präsident Mahinda Rajapaksa und Gesundheitsminister Maithripala Sirisena (links)
Wagombea wa urais, Mahinda Rajapaksa wa sasa (kushoto), na mpinzani wake Maithripala SirisenaPicha: picture-alliance/AP//E. Jayawardena

Kiongozi huyo wa muda mrefu zaidi katika kanda ya Asia Kusini, alionekana kama mtu asieshindika kisiasa baada ya ushindi huo dhidi ya Tamil Tigers mwaka 2009. Lakini mambo yanaonekana kuwa magumu kwake

Rajapaksa alishinda kwa kishindo katika uchaguzi wa mwaka 2010, lakini wakosoaji wanasema kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 69 ameshindwa kuleta maridhiano na kabila la wachache la Tamil katika miaka iliyofuatia.

Mgombea wa upinzani Mithripala Sirisena akiwapungia wafuasi wake wakati wa kampeni.
Mgombea wa upinzani Mithripala Sirisena akiwapungia wafuasi wake wakati wa kampeni.Picha: Reuters/Stringer

Muhula wake wa pili uligubikwa na tuhuma za rushwa, ikiwemo kudhoofisha uhuru wa mahakama, na kutoa upendeleo kwa washirika wake wa kisiasa kwa kuwapa kandarasi nono.

Maithripala Sirisena abadili upepo

Uamuzi wa kushtukiza wa waziri wake wa afya Maithripala Sirisena kujitoa katika chama tawala na kusimama kama mgombea wa upinzani, umegeuza kile kilichoonekana awali kama kuteleza kwenye barafu na kuwa kampeni ya ushindani wa kweli. Paikiasothy Saravanamuttu, mkurugenzi wa kituo cha uchambuzi wa sera, alisema ushindani utakuwa mkali katika uchaguzi huo.

"Uchaguzi huu ni wa kihistoria na wenye maamuzi kwa sababu hii ndiyo mara ya kwanza kwa rais kugombea mhula wa tatu. Lakini nadhani jambo muhimu zaidi ni kwamba kuna uwezekano mkubwa wa muundo na utamaduni wa kisiasa kubadilika," alisema Saravanamuttu na kuongeza kuwa ni dhahiri utawala wa Rajapaksa ni wa kidikteta, na mradi wa kifalme. "Utaondoka kutoka kwenye utamaduni wa bunge na demokrasia kwenda kwenye utawala wa mkono wa chuma."

Mchambuzi wa siasa Victor Ivan, alisema Sirisena, ambaye hapo awali alikuwa hafahamiki sana, amegeuka kuwa ishara ya kuchukizwa kwa raia na rushwa iliyokithiri. Ivan aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP, kuwa Rajapaska ameshindwa kuhakikisha maridhiano, na badala yake ameelekeza nguvu zake kwenye ujenzi wa barabara na bandari. Ingawa hayo yalikuwa mazuri kwa ukuaji wa pato la jumla la ndani, Ivan anasema hayatoshi kuiponya jamii iliyojeruhiwa na mgogoro wa miongo kadhaa.

Rais Mahinda Rajapaksa akiwa na rais wa China Xi Jinping. China ni mwekezaji mkubwa nchini Sri Lanka.
Rais Mahinda Rajapaksa akiwa na rais wa China Xi Jinping. China ni mwekezaji mkubwa nchini Sri Lanka.Picha: Dinuka Liyanawatte/Reuters

Uchumi wa Sri Lanka umekuwa kwa wastani wa asilimia saba kila mwaka tangu kumalizika kwa vita, ukichangiwa kwa sehemu na uwekezaji mkubwa wa mshirika wa karibu wa Rajapaska, China. Lakini wapinzani wanasema makandarasi wa Kichina wameajiri wenyeji wachache tu, na pato la kaya halijakuwa sambamba na ukuaji wa kitaifa.

Kama kacheza sivyo karata zake

Vyama vya upinzani, kikiwemo chama kikuu cha Tamil vimemuunga mkono Sirisena, mkulima mwenye umri wa miaka 63 aliegeuka mwanasiasa, ambaye anatokea katika Jamii ya kabila la Sinhale walio wengi. Wakati anaendelea kuwa na uungwaji mkono miongoni mwa wapigakura wa Sinhale, Rajapaksa anachukiwa sana na watu wa jamii kubwa zaidi ya walio wachache, ambao wanachangia asilimia 13 ya raia milioni 15 wa Sri Lanka, na ambao mara nyingi hupiga kura kama kundi.

Rajapakse aliitisha uchaguzi wa mapema miaka miwili kabla ya wakati akitumai kuwapiga chenga wapinzani. Washirika wake wa karibu wanasema uamuzi huo ulifanywa kwa sehemu kufuatia ushauri wa manjimu wake. Rais huyo aliondoa ukomo wa mihula na kujipa mamlaka zaidi mara baada ya kushinda mhula wa pili mwaka 2010.

Rais wa Zamani wa Sri Lanka na hasimu mkubwa wa Rajapaksa, Chandrika Kumarutunga.
Rais wa Zamani wa Sri Lanka na hasimu mkubwa wa Rajapaksa, Chandrika Kumarutunga.Picha: picture-alliance/AP/Vincent Thian

Kujiondoa kwa Sirisena katika chama tawala kulipangwa kwa ustadi mkubwa na hasimu wa Rajapakse, rais wa zamani Chandrika Kumaratunga, ambaye alirejea katika siasa baada ya kustaafu kwa miaka tisa, na amekigawa chama tawala. Chama chenye msimamo mkali cha watawa wa Kibudha wa Sinhale, ambacho kilimshangilia Rajapakse kwa kukataa kukubali uchunguzi wa kimataifa, kilijiunga na upinzani mwezi Novemba, kikimtuhumu kwa rushwa iliyokithiri na upendeleo.

Vyombo vya habari vinavyolemea upande wa serikali vimetabiri mpambano mkali, wakati wanadiplomasia mjini Colombo wamesema wanaona uwezekano wa matokeo kuelekea upande wa upinzani.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe
Mhariri: Daniel Gakuba