1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nani atatamba kati ya Bayern Munich na Real Madrid?

John Juma
25 Aprili 2018

Bayern Munich kuchuana na Real Madrid uwanjani Allianz Arena katika mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa

https://p.dw.com/p/2wei1
25.04.2018 Champions League: Bayern München gegen Real Madrid
25.04.2018 Fussball Champions League/ Hinspiel FC Bayern Muenchen gegen Real Madrid
Picha: picture-alliance/S. Simon

Mtanange wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa kati ya Bayern Munich na Real Madrid utakuwa mchuano wa kupigania pia ubabe wa soka la Ulaya. Kidumbwedumbwe hicho cha kwanza kati ya timu hizo mbili ni leo katika uga wa Allianz Arena.

Hii itakuwa mara ya 25 kwa timu hizo mbili kukutana katika soka la Ulaya, huku kila timu ikiwa imeshinda mara 11 na kutoka sare mara mbili. Leo usiku itakuwa mara ya saba kwa vilabu hivi kukutana katika nusu fainali. Katika mapambano yao yote, Real Madrid imefunga jumla ya mabao 37, Bayern mabao 36. 

Kocha wa Bayern Munich Jupp Heynckes amesema Real Madrid inapaswa kuwa na wasiwasi kuhusu Robert Lewandowski kama vile ambavyo Bayern Munich itakuwa inalenga kumdhibiti Cristiano Ronaldo.

Mabingwa hao wa Ujerumani wanawaalika Real katika mechi kali ya miamba ya Ulaya wakilenga kutwaa mataji matatu msimu huu. Bayern imethibitisha kuwa David Alaba hatashiriki mechi ya leo kutokana na jeraha la paja.

Macho wa Cristiano Ronaldo

Ronaldo amefunga mabao 42 katika mechi 39
Ronaldo amefunga mabao 42 katika mechi 39Picha: Reuters/P. Hanna

Ronaldo amefunga mabao 42 katika mechi 39 wakati Lewandoswki ametikisa wavu mara 39 katika mechi 43. Mechi ya marudio ya nusu fainali kati ya timu hizo mbili itakuwa Mei mosi mjini Madrid.

Uchambuzi wa awali hasa umemlenga mshambuliaji wa Real Madrid Cristiano Ronaldo ambaye amefunga bao katika kila mechi zote 10 za Madrid katika Ligi ya Mabingwa msimu huu.

Amefunga mabao 9 katika mechi sita dhidi ya Bayern Munich.

Hata hivyo kocha wa Real Madrid Zinedine Zidane ameonya kuwa Bayern Munich wako imara wakati huu kuliko walipowabandua nje ya kinyang'anyiro hicho msimu uliopita.

Zidane amesema kuwa watahitaji kuonyesha uchezaji wa kiwango cha juu dhidi ya Bayern, huku akiongeza kuwa suala kuwa waliwaondoa katika robo fainali msimu uliopita halijalishi lolote wakati huu.

Hapo jana, Liverpool iliwachabanga Roma mabao matano kwa mawili katika mechi ya kusisimua iliyochezwa uwanjani Anfield. Nyota wa Liverpool Mohamed Salah alifungia timu yake mabao mawili miongoni mwa mabao hayo matano na kuonesha umahiri wake.

Mwandishi: John Juma/RTRE/AFPE

Mhariri: Iddi Ssessanga