1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NAIROBI: Kundi la waasi la LRA la Uganda lamshutumu Rais wa kusini mwa Sudan, Salva Kiir.

25 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCY0

Waasi wa kundi la Lord´s Resistance Army leo wamemshutumu rais wa kusini mwa Sudan, Salva Kiir kwa kuchochea ghasia dhidi yao kwa taarifa aliyotoa gazetini kama atakabiliana nao vikali.

Waasi hao wamekuwa wakishiriki kwenye mazungumzo ya amani kati yao na serikali ya Uganda yaliyosimamiwa na serikali ya kusini mwa Sudan tangu mwezi Julai mwaka uliopita.

Mwezi huu kundi hilo liliyasusia mazungumzo hayo katika mji wa Juba likidai kwamba lilichelea kushambuliwa na wanajeshi wa Sudan.

Gazeti la Monitor, nchini Uganda limesema Salva Kiir alitoa taarifa hiyo kwa lugha ya kiarabu wakati alipozuru eneo la kusini mwa Sudan jumanne iliyopita.

Salva Kiir amenukuliwa akisema kundi la LRA ni tishio kwa raia wala si jukumu la SPLA peke yake bali kila mwenye bunduki anapaswa kuwasaka na kuwaua waasi hao.

Habari hiyo za Salva Kiir zimetolewa punde baada ya Rais wa Sudan, Hassan Omar al-Bashir kuapa kwamba atalifurusha kundi la LRA kutoka Sudan.