1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Thailand, sio mwisho.

Miraji Othman3 Desemba 2008

Mfalme wa Thailand kimya juu ya mzozo katika nchi yake.

https://p.dw.com/p/G8TB
Uwanja wa ndege wa Bngkok umefunguliwa tena leo. Ndege ya kwanza ya Shirika la Ndege la Thailand inaruka.Picha: AP


Ndege ya kwanza ya kimataifa imeondoka Bangkok leo baada ya kiwanja kikuu cha ndege katika mji mkuu huo wa Thailand kuachwa kuzingirwa na waandamanaji. Lakini hio haina maana kwamba mzozo wa kisiasa wa nchi hiyo umemalizika. Kuzingirwa uwanja huo wa ndege kwa wiki kulimalizika jana baada ya Muungano wa Umma kwa ajili ya Demokrasia ulipodai ushindi dhidi ya serekali ya waziri mkuu Somchai Wongsawat pale mahakama ilipompiga marufuku waziri mkuu huyo asishiriki katika siasa na kukupiga marufuku chama tawala. Watalii sasa wamepumua

Baada ya mahakama ya katiba ya Thailand kukipiga marufuku chama tawala na waziri mkuu akajiuzulu, basi waandamanaji waliacha kuuzingira uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Bangkok. Na hayo yalifanyika bila ya polisi kutumia nguvu. Lakini yaonesha mambo hayajabadilika katika kupimana nguvu bungeni. Pale wafuasi wa Muungano wa Umma watakaporejea majumbani na kutafakari juu ya maandamano yao yaliodumu miezi, basi watatahamaki na kuona kwamba kambi ile ile ya kisiasa ya zamani bado iko madarakani. Na nini kitakachokuja, mtu anaweza kukiwaza.

Wapinzani wa serekali watahisi kwamba vitendo vyao visivokuwa vya kisheria vimekubalika kutokana na uamuzi wa mahakama ya katiba, na kwamba maandamano yao ya miezi yamewaletea mafanikio. Dola haijatumia nguvu kuwazuwia walio wachache wasiyatambuwe matokeo ya uchaguzi wa kidemokrasia, hivyo kuwalazimisha wa-Thailand walio wengi waufute msimamo wa walio wachache.

Wapinzani kukikalia kiwanja cha ndege lilikuwa sio jambo lolote isipokuwa ni utumiaji wa mabavu na jni kitendo kisichokuwa cha haki kwa wananchi wa Thailand. Biashara ya utalii ambayo inachangia kukubwa katika uchumi wote wa nchi hiyo, ulitumiwa vibaya kama silaha katika mchezo huo. Inakisiwa idadi ya watalii watakaokwenda Thailand mwakani itakuwa nusu ya ile ya kawaida. Na hali hiyo itatokea, kwa vyovyote, katika wakati ambao lazima itazamiwe hali hiyo mbaya. Mtu anakisia kwamba nafasi milioni moja za kazi zitapotea katika sekta ya utalii.

Mahakama ya kikatiba sasa imegundua kwamba mfumo wa vyama vya kisiasa umeuzika mfumo wa kidemokrasia katika nchi hiyo, lakini mahakama yenyewe imesaidia katika kuweko hali hiyo. Ilivibariki baadae vitendo visivokuwa na dhamana vya watu walioukalia uwanja wa ndege. Malalamiko ya kununuliwa kura katika uchaguzi ni makubwa na heunda yanaweza kuwa yalifanywa na vyama vyote vya kisiasa vya Thailand, pindi mtu atafanya uchunguzi wa kina. Katika jamii ambako pengo baina ya wale watu walio na neema katika miji na wale walio maskini vijijini ni kubwa mno, ambapo mtu mzito wa kifedha huko Bangkok anaweza kujinunulia wingi wa wabunge, katika jamii kama hiyo ni muhimu yachukuliwe maamuzi makubwa zaidi kuliko tu kukipiga marufuku chama cha siasa.

Nchini Thailand kumezuka mapambano ya kitabaka baina ya watawala wa zamani, wafanya biashara na wasomi wa kutokea Bangkok ambao pamoja na wenye kupendelea ufalme wanahofia kupoteza madaraka yao ya kisiasa pale wananchi wa kawaida kutoka mashambani watakapopata kweli haki zao za kisiasa. Na wananchi wa kawaida watauona uamuzi huu wa mahakama kama njama ya wale walio na madaraka; hawatavutiwa na jambo hilo. Kwa upande mwengine, ule unaoitwa Muungano wa Umma kwa ajili ya Demokrasia umeionesha nchi na dunia nzima nini anachoweza mtu kukifikia pale anapokuwa na azma ya kweli na kusema YAMETOSHA.

Na pale anapoungwa mkono na kufadhiliwa na watu barabara. Lakini hakuna kinachosemwa juu ya wale watu waliokuwa nyuma ya ule umma ulioukalia uwanja wa ndege. Kwani huko Thailand kuna sheria ambayo inampeleka mtu gerezani pindi atamtukana Mfalme wa nchi hiyo. Jana mfalme huyo alitoa hotuba katika paredi ya kijeshi ya kila mwaka, lakini mfalme huyo aliyetawala kwa muda mrefu kabisa kuliko mfalme yeyote duniani, hajaona iko haja ya kuutaja mzozo ulioko katika nchi yake. Demokrasia huko Thailand imekufa, lakini mfalme anaishi.