1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa mashariki ya Kati wazuka upya

Eric Kalume Ponda22 Desemba 2008

Kundi la Wapiganaji wa Kipalestina la Hamas ambalo siku ya Ijumaa lilianzisha mashambulizi mapya dhidi ya Israel kudai uhuru kamili wa eneo la ukanda wa Ghaza, limetangaza muda wa masaa 24 kusitisha mashambulizi.

https://p.dw.com/p/GLWX
Wanajeshi wakishika doria katika moja wapo ya kizuizi cha barabarani kati ya Israel na Ukanda wa GhazaPicha: pIcture-alliance/ dpa



Hata hivyo lakini kundi hilo limetisha kufanya mashambuli zaidi iwapo Israel itatekeleza vitisho vyake vya kulipiza mashambulizi ya mwishoni mwa wiki.


Wapiganaji wa kundi la Hamas walianzisha mashambulizi mapya baada ya kumalizika kwa mkataba wa miezi sita ijumaa iliyopita ulioafikiwa baina ya pande hizo mbili na kutangaza kuwa hawataongeza muda wa mktaba huo.

Hayo yote yakiendelea viongozi wa Israel wamo katika harakati ya kutafuta kuungwa mkono dhidi ya vitindo vya wapiganaji hao wa Hamas.


Wapiganaji wa Hamas walichukua hatua hiyo kufuatia ombi la serikali ya Misri ili kutoa nafasi ya kupelekwa kwa misaada katika eneo la Ukanda wa Ghaza.


Wapiganaji hao wa Hamas jana jumapili walifanya mashambulizi ya mizinga ya roketi dhidi ya Israel, hali iliyopelekea Israel kujibu kwa mashambulizi ya angani katika eneo hilo la Mpakani yaliyosababisha kifo cha mpiganaji mmoja na raia kujeruhiwa.


Hali ya wasi wasi inazidi kutanda katika eneo hilo la mpakani tangu kumalizika kwa muda wa kudumishwa mkataba wa kusitisha mashambulizi baina ya pande hizo mbili siku ya Ijuma. Mzozo wa hivi punde unatishia usalama wa eneo hilo ambalo limekuwa na hali ya utulivu tangu wapiganaji hao kujipatia uhuru mwaka 2007.


Kundi la Hamas linatisha kufanya mashambulizi ya kujitolea mhanga katika ardhi ya Israel iwapo itaendelea kufanya mashambulizi ya angani katika maeneo yake. Mara ya mwisho kwa kundi la Hamas kufanya mashambulizi ya kujitolea mhanga dhidi ya Isarael ni mwaka wa 2005.


Afisa wa utawala wa Kipalestina Anyman Taha, alisema kuwa muda huo wa kusitisha mashambulizi huenda utaongezwa iwapo Israel itakomesha mashambulizi ya angani na kuondoa vikwazo dhidi ya eneo hilo la Ukanda wa Ghaza.


Msemaji wa jeshi la Israel alidai kuwa wapiganaji hao wa Hamasi walirusha makombora mawili na mzinga wa Roketi dhidi ya vituo mpakani vya Israel.

Huku hayo yakijiri, viongozi wa Israel wametoa onyo kali kwamba haitasita kujibu mashambulizi ya wapiganaji wa Kundi la Hamas.


Waziri wa mambo ya nje wa Israel Tzipi Livni ambayi ni kiongozi wa chama tawala cha KADIMA, amewaagiza mabalozi wa Israel kote ulimwenguni, kusisitiza kuwa Israel haitasita kujibu mashambulizi dhidi yake katika eneo la mpakani.


Matamshi kama hayo pia yametolewa na kiongozi wa upinzani Benjamin Netanyahu.


Wakati huo huo kiongozi wa Palestina Mahmud Abbas yuko nchini Urusi kukutana na Rais Dmitry Medvedev, kutafuta kuungwa mkono katika juhudi zake za kuendeleza mpango wa amani wa eneo la mashariki ya kati.


Kadhalika kiongozi huyo amepangiwa kukutana na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov, kujadilia hali ilivyo katika eneo hilo la mashariki na kuhimiza jamii ya kimataifa kuishinikiza Israel kukomesha ujenzi wa makazi mapya katika eneo hilo la ukanda wa Ghaza mbali na kuondoa vizuizi vya barabarani kabla ya kurejelewa kwa mashauriano yoyote ya kutafuta amani.


Kwa upande wake, waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert amepangiwa kufanya mazungumzo na kiongozi wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, kutafuta uwezekano wa taifa hilo iwapo linaweza kuwa mpatanishi kwenye mzozo baina yake na Syria.


Mataifa hayo mawili yamekuwa na uhasama tangu mwaka wa 1948. Huenda hizi ni juhudi za dakika za mwisho mwisho kwa kiongozi huyo wa Israel aliyejiuzulu kabla ya kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu nchini humo.


Olmert alijiuzulu kufuatia kashfa ya ufisadi, ingawa ataendelea kuhudu hadi pale serikali mpya itakapoundwa baada ya uchaguzi huo mwezi February.


Hata hivyo juhudi hizo zimepuziliwa mbali na mpinzani wake Benjamin Netanyahu akisema kuwa mkataba wowote utakaoafikiwa hautatambuliwa na serikali yake iwapo atachaguliwa kuliongoza taifa hilo.