1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa mashariki ya kati Israel na Hezboullah zajibizana.

Sekione Kitojo10 Agosti 2009

Israel imeonya leo kuwa serikali ya Lebanon itachukua jukumu la shambulio lolote dhidi yake litakalofanywa na Hezboullah iwapo kundi hilo litajumuishwa katika serikali.

https://p.dw.com/p/J76T

Israel imeonya leo kuwa serikali ya Lebanon kwa jumla italaumiwa kwa shambulio lolote kutoka katika ardhi yake iwapo kundi la wanamgambo wa Kishia la Hezboullah litakuwa sehemu ya serikali mpya ya nchi hiyo. Nae waziri wa mambo ya kigeni wa Israel amesema kuwa kuimarisha usalama na uchumi wa Palestina ndio pekee vitu ambavyo mazungumzo ya amani ya mashariki ya kati yanaweza kufanikisha katika miaka inayokuja, akionya dhidi ya jaribio la kulazimisha kupatikana makubaliano.

Iwapo Hezboullah itajumuishwa katika serikali itakuwa wazi kwamba serikali ya Lebanon itawajibika na shambulio lolote litakalofanywa kutoka katika ardhi yake dhidi ya Israel, amesema waziri mkuu Benjamin Netanyahu.

Kumekuwa na hali ya kuongezeka kwa vita vya maneno katika siku za hivi karibuni kati ya Israel na Hezboullah , pande zilizopigana vita vya siku 34 katika mwaka 2006 ambapo watu 1,200 wamepoteza maisha yao, wengi wao wakiwa raia, nchini Lebanon na 160 nchini Israel, wengi wao wakiwa wanajeshi.

Jana Jumapili naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Israel Dany Ayalon ameionya Hezboullah dhidi ya kuwashambulia raia wa Israel baada ya ripoti kuwa Misr imegundua mpango unaotayarishwa na kundi linalohusiana na al-Qaeda kumuua balozi wa Israel nchini Misr.

Hapo mapema kiongozi wa ngazi ya juu wa Hezboullah amesema kuwa shambulio lolote la Israel dhidi ya Lebanon litajibiwa kwa nguvu zote kutoka Hezboullah kuliko ilivyokuwa mwaka 2006.

Wakati huo huo chama cha rais wa Palestina Mahmoud Abbas cha Fatah kimekuwa kikichagua viongozi wake wapya kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka 20 leo Jumatatu, katika matumaini kuwa kinaweza kujiimarisha baada ya kudhoofishwa na mivutano ya ndani pamoja na kufurushwa kutoka katika ukanda wa Gaza na mahasimu wao chama cha Hamas. Mbunge wa chama cha Fatah Sami Abu-Zuhri kutoka eneo la Gaza amesema., kuwa kuchaguliwa kwa Mahmoud Abbas kuwa kiongozi wa Fatah kulikuwa ni suala wasi wasi. Lakini ukitathmini hatua ya kuondolewa na Hamas katika ukanda wa Gaza, uamuzi wa Fatah haujakuwa wa maana. Kuporomoka kwa Fatah kutakuwa kumeongezeka zaidi.

Zoezi la kuhesabu ya kura lililopangwa kuanza leo Jumatatu asubuhi liliahirishwa kuwawezesha wanachama wengi zaidi kutoka ukanda wa Gaza kupiga kura zao kwa simu na zoezi hilo limepangwa kuanza mchana ama jioni leo. Maelfu ya wanachama wa Fatah walipiga kura zao kwa simu kwa kuwa mahasimu wao Hamas , wanaounda serikali katika ukanda wa Gaza , waliwazuwia kuhudhuria upigaji kura huko katika ukingo wa magharibi.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Israel Avigdor Liebermann amewaambia wabunge wa chama cha Democratic kutoka Marekani leo kuwa msimamo mkali usiokubali maridhiano wa Wapalestina kuhusu mji wa Jerusalem, haki ya wakimbizi kurejea katika maeneo yao pamoja na maeneo ya makaazi ya walowezi wa Kiyahudi yanaonekana kuleta mwanya usiozibika kati ya Israel na Wapalestina.

Mwandishi Sekione Kitojo /AFPE

Mhariri Mohamed Abdul-Rahman.

►◄