Mzozo wa kinuklea wa Korea ya kaskazini-nini la kufanya? | Habari za Ulimwengu | DW | 24.10.2006
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

Mzozo wa kinuklea wa Korea ya kaskazini-nini la kufanya?

Sera zinazotofautiana za Marekani na Korea ya kusini zimeshindwa kuitia kishindo Korea ya kaskazini

Maandamano mjini Seoul kupinga hatua kali dhidi ya Korea ya kaskazini

Maandamano mjini Seoul kupinga hatua kali dhidi ya Korea ya kaskazini

Sera za kirafiki za Korea ya kusini kuelekea Korea ya kaskazini zililengwa kuishawishi Pyongyang iregeze kamba.Msimamo mkali wa Mkali wa Marekani ulilenga hay ohayo.Hakuna kilichofanikiwa.Sasa dawa iko wapi?

Wadadisi wanasema Korea ya kusini na Marekani,ingawa ni marafiki wa dhati,lakini wamekataa kushirikiana katika kubuni mkakati wa pamoja, mtindo wa kutafuna na kupuliza ili kuitanabahisha Pyongyang.

Katika wakati ambapo rais Roh Moo-Hyun wa Korea ya kusini anapania kuendelea kuisaidia Korea ya kaskazini, na mwenzake wa Marekani,George w. Bush anashikilia msimamo mkakamavu dhidi ya utawala wa Pyongyang,matumaini ni haba ya kuweza kufikia mmaridhiano katika mzozo wa kinuklea-wadadisi hao wanasema.

“Panahitajika maridhiano kati ya Washington na Seoul kabla ya kutaraji maendeleo ya aina yoyote kupatikana pamoja na Korea ya kaskazini” amesema hayo Peter Beck wa shirika la kimataifa la kumaliza mizozo-International Crisis Group.

“Tatizo kubwa lililoko limetokana na kushindwa serikali zetu kukubaliana“ amesema hayo bwana Beck katika warsha moja hapo jana.Ameongeza kusema kinachokosekana ni „utaratibu wa kupuliza na kutafuna“.

Korea ya kusini inasisitiza miradi miwili ya ubiya itaendelea katika eneo la mpakani-licha ya kuwapatia Korea ya kaskazini dala karibu bilioni moja tangu mwaka 1998-fedha ambazo pengine Pyongyang imezitumia ili kutengeneza bomu la kinuklea.

Wakosoaji wanahisi msimamo wa Roh wa kuwajibika bila ya masharti ndio unaowapa kichwa viongozi wa Pyongyang waendelee kuamini hakuna lolote litakalotokea.

Korea ya kaskazini hivi karibuni imefanya jaribio la kinuklea.Ikiwa hamjajitayarisha kuzuwia tangu sasa misaada mnayotoa kwa Korea ya kaskazini,mnafikiria kufanya hivyo lini? Anajiuliza PAIK Jin-Hyun wa chuo kikuu cha taifa mjini Seoul. Seoul National University.

Amesema miradi ya ubiya inabidi isitishwe kwasababu sera za kutanguliza mbele nia njema zimeshindwa.

“Hazitasaidia kitu,hazijasaidia chochote miaka ya nyuma” amesema Peck.

Lakini katika wakati ambapo Seoul inadhihirika kuwajibika,Marekani inaonyesha haiko tayari kuregeza kamba-hata ikiwa kwa kufanya hivyo pengine itaishawishi Korea ya kusini iridhie na kufuata msimamo mkali.

Beck anashadidia juu ya hofu za Korea ya kusini kwamba hatua kali zinaweza kuepelekea kung’oka madarakani utawala na hivyo kuuitwika mzigo mkubwa zaidi Korea ya kusini wa kuwashughulikia mamilioni ya wakorea ya kaskazini waliofilisika kifedha na kitamaduni.

Kuna hofu pia kwamba hatua kali zitaufanya mzozo uzidi makali.“Kila tunapoitia kishindo Korea ya kaskazini ndipo nao wanapozidi kufuata msimamo shupavu na wa hatari.”

Park Young-Ho wa taasisi inayoshughulikia masuala ya muungano wa taifa anasema utayarifu wa Marekani wa kuendeleza mazungumzo ya ana kwa ana pamoja na Korea ya kaskazini-shauri lililokua likitolewa kila kwa mara na Pyongyang huenda ukasaidia kupunguza hofu za waKorea ya kusini.

Wadadisi wanakubaliana lakini kwamba hakuna mabadiliko yatakayotokea kabla ya serikali kubadilika nchini Korea ya kusini na Marekani pia.Rais mpya wa Korea ya kusini atachaguliwa mwakani na nchini Marekani ,rais atachaguliwa mwaka 2008.

 • Tarehe 24.10.2006
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CBI6
 • Tarehe 24.10.2006
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CBI6

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com