1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Iran waendelea kutokota

Bruce Amani
2 Januari 2018

Karibu watu 12 wameuawa katika maandamano yanayoendelea nchini Iran, na waandamanaji walio na silaha wamejaribu kuvamia vituo vya polisi na jeshi. Maandamano hayo yalianza Alhamisi na kusambaa kwenye miji mbalimbali

https://p.dw.com/p/2qBjY
Iran Protest in Teheran
Picha: Fars

Maandamano hayo yalianza Alhamisi katika mji wa Mashhad kuhusiana na masuala ya kiuchumi na yakasambaa hadi miji mingine, huku baadhi ya waandamanaji wakipiga kelele za kuipinga serikali na kiongozi mkuu Ayatollah Ali Khamenei. Mamia ya watu wamekamatwa.

Televisheni ya taifa imesema watu 10 wameuawa Jumapili usiku, bila kufafanua. Waandamanaji wawili waliuawa wakati wa maandamano katika mji wa magharibi mwa Iran Jumamosi usiku.

Televisheni imesema baadhi ya waandamaanaji walijaribu kuviteka vituo vya polisi na jeshi lakini wakakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa vikosi vya usalama. Hata hivyo televisheni hiyo haijasema kulikotokea mashambulizi hayo.

Iran Protest in Teheran
Vurugu zimesambaa katika miji kadhaa kote IranPicha: Irane-ma

Televisheni ya taifa ilionyesha picha za majengo yanayochomeka, pamoja wahudumu wa matibabu ya dharura wakijaribu kumpa huduma ya kwanza mtu mmoja aliyejeruhiwa. Pia ilionyesha lori la zimamoto ambalo lilionekana kushambuliwa na kuchomwa moto. Televisheni ya taifa imesema watu sita waliuawa katika mji wa magharibi wa Tuyserkan, kusini magharibi mwa mji mkuu Tehran. Ilisema wengine watatu waliuawa katika mji wa Shahinshahr, kusini mwa Tehran. Haikusema alikouawa mtu wa kumi.

Mapema leo, mwakilishi wa mji wa Izeh alisema watu wawili waliuawa mjini humo Jumapili usiku. Jana Jumapili, Iran ilizuia huduma za Instagram na Telegram ambazo zinatumiwa na wanaharakati wanaoandaa maandamano hayo. Rais Hassan Rouhani amekiri kuhusu hasira ya umma kuhusiana na hali mbaya ya uchumi wa taifa hilo la kiislamu ijapokuwa yeye na wengine wameonya kuwa serikali haitasita kuwakabili wanaozingatiwa kuwa wavunja sheria.

Rais wa Marekani Donald Trump ambaye amekuwa akiandika ujumbe wa Twitter akiwaunga mkono waandamanaji nchini Iran, ameendeleza katika hotuba yake ya kuukaribisha Mwaka Mpya, akiitaja nchi hiyo kuwa "inayoshindwa katika kila ngazi licha ya makubaliano mabaya yaliyofikiwa kati yao na utawala wa Obama”.

"Watu wa Iran wameumizwa kwa miaka mingi,” aliandika. "Wana njaa ya chakula na ya uhuru. Pamoja na haki za binaadamu, mali za Iran zinaporwa. Ni wakati wa Mabadiliko!”

Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Caro Robi