1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo Mashariki ya Kati wapamba moto

Amina Mjahid16 Julai 2014

Israel leo imeendelea na mashambulizi yake dhidi ya wanamgambo wa Kipalestina wa chama cha Hamas, katika Ukanda wa Gaza baada ya kushindwa juhudi za Misri, kuzitaka pande hizo mbili husika kusimamisha mapigano.

https://p.dw.com/p/1Cdrf
Athari ya mashambuliui ya angani katika ukanda wa Gaza
Athari ya mashambuliui ya angani katika ukanda wa GazaPicha: picture alliance/ZUMA Press

Israel pia imewaambia maelfu ya wakaazi walio mpakani mwa Gaza kuondoka kufuatia mashambulizi zaidi inayoendelea kutekeleza.

Wakaazi Kaskazini mwa miji ya Beit Lahiya, Zeitoun na Shijaiyah ilio karibu na mpaka wa Israel, wamepokea Simu, Ujumbe na Vijikaratasi vinayvoeleza waondoke katika maeneo hayo kuanzia saa mbili hii leo asubuhi au watashambuliwa.

Israel imesema inazilenga nyumba 30 zikiwemo zile za wakuu wa wanamgambo walio na msimamo mkali wa Hamas wakiwemo, Mahmoud Zahar, Jamila Shanti, Fathi Hamas na Ismail Ashkar.

Kulingana na wataalamu wa afya wa Palestina, Idadi ya vifo vya wapalestina ndani ya siku tisa tangu Israel ianzishe mashambulizi yake dhidhi ya Ukanda wa Gaza, ni zaidi ya 200 huku watu 1,450 wakiachwa na majeraha mabaya.

Upande wa Israel ni mtu mmoja tu aliyeuwawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa tangu kuanza kwa mapigano Julai 8, huku wapalestina wakirusha maroketi kuelekea ardhi ya Israel, kutokea Gaza.

Wanawake na watoto waliohama makaazi yao kufuatia agizo la Israel
Wanawake na watoto waliohama makaazi yao kufuatia agizo la IsraelPicha: Mahmud Hams/AFP/Getty Images

Mabomu yalianza tena kuangushwa ukanda wa Gaza siku moja baada ya Israel kukubali pendekezo la Misri la kusimamisha uhasama unaoendelea.

Hatua hiyo ilitarajiwa kufuatiwa na mazungumzo yaliolenga kupatikana kwa suluhu ya muda mrefu ya kusimamisha mapigano.

Lakini Hamas ikaukataa mpango huo na kundelea kurusha mabomu nchini Israel.

Hamas italipa kwa kukataa kusimamisha mapigano asema Netanyahu

Huku juhudi za Misri zikivunjika, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameonya kuwa Hamas watalipa kwa kukataa pandekezo la kusimamisha mapigano.

"Ingekuwa vyema iwapo tungesuluhisha hali ilivyo kwa njia ya kidiplomasia, na tumejaribu kufanya hivyo kwa kukubali pendekezo la Misri la kusimamisha mapigano, lakini Hamas haijatupa njia nyengine ila kuendelea kutanua na kuzidisha kampeni yetu dhidi yao," amesema Benjamin Netanyahu.

Wakati huo huo shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch limesema Israel ni lazima isimamishe hujuma zake kwa wakaazi wa Ukanda wa Gaza. Shirika hilo limesema tangu kuanza mapigano wanaouwawa na kuathirika zaidi ni wanawake na watoto.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais wa Palestina Mahmood Abbas
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais wa Palestina Mahmood AbbasPicha: CHRIS KLEPONIS/AFP/Getty Images

Mkurugenzi wa Mashariki ya Kati wa shirika hilo llililo na makao yake makuu mjini New York Marekani, Sarah Leah Whitson pia amewataka wanamgambo wa Hamas kuacha kuishambulia Israel.

Rais wa Palestina Mahmoud Abbas anatarajiwa kwenda Misri hii leo kwa mazungumzo juu ya kusimamisha mapigano yanayoendelea.

Mwandishi Amina Abubakar/AP/dpa

Mhariri Mohammed Abdul-Rahman