1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanajeshi wa Marekani auwawa Irak Gates asifu kuimarika kwa usalama

11 Februari 2008
https://p.dw.com/p/D5tK

Mabomu mawili yaliyokuwa yametegwa ndani ya gari mjini Baghdad nchini Irak yamewaua watu wasiopungua wawili na kuwajeruhi wengine watano.

Milipuko hiyo imetokea saa chache baada ya waziri wa ulinzi wa Marekani, Robert Gates, kusema usalama umeimarika nchini Irak.

Akiwa katika ziara ya siku mbili nchini humo, Robert Gates amesema mapema leo kwamba anaounga mkono wazo la kusitisha kwa muda kupunguza idadi ya wanajeshi wa Marekani nchini Irak mara tu mpango wa kuviondoa vikosi vitano vya jeshi la Marekani utakapokamilika ifikapo mwezi Julai mwaka huu.

Mashambulio yamepungua kwa asilimia 60 tangu mwezi Juni mwaka jana, lakini makamanda wa jeshi la Marekani wanasema kundi la al Qaeda, linalolaumiwa kwa mashambulio makubwa ya mabomu, bado linabakia kuwa adui hatari.

Zaidi ya watu 50 waliuwawa kwenye wimbi la mashambulio ya mabomu hapo jana nchini Irak.

Mwanajeshi mmoja wa Marekani aliuwawa jana na wengine wawili kujeruhiwa wakati bomu lililokuwa limetegwa kando ya barabara lilipoilipua gari ya jeshi la Marekani katika mkoa wa Diyala.