1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yamkamata kiongozi wa waasi.

Abdu Said Mtullya23 Februari 2010

Mwanaitikadi kali wa kisunni akamatwa na Iran.

https://p.dw.com/p/M9Ml
Bendera za Iran na Pakistan.ishara ya urafiki?

Maafisa wa Iran wamearifu kuwa wamemkamata kiongozi wa wanaitikadi kali wa kisunni  wakati akiwa ndani ya ndege .

Mtu huyo Abdolmalek Rigi  anaongoza kundi la wapiganaji wa Jundallah-yaani  askari  wa Mungu.

Iran inasema  ilimkamata Abdolmalik Rigi saa 24 baada kuwapo kwenye kituo  cha kijeshi cha Marekani nchini  Afghanistan.

Iran imesema kukamatwa kwa mtu huyo ambae ni kiongozi wa wanaitikadi kali wa kisunni ni pigo kwa maadui  wake wakubwa wa magharibi.

Waziri wa upelelezi wa Iran  bwana Heydar Moslehi anadai  kwamba Marekani ilimpa Rigi pasipoti ya kiafghani  na  kwamba  alifika hadi Ulaya na kukutana na mkuu wa kijeshi wa NATO.

Lakini Marekani imekanusha madai hayo na kuyaita kuwa ni uzushi.

Katika orodha ya watu   wanaotafutwa na Iran, Abdolmalek Rigi alikuwa katika  nafasi ya kwanza.

Kiongozi huyo wa kundi la waasi linaloitwa Jundallah yaani askari wa Mungu  amekuwa anapelembwa  kwa muda  wa miezi mitano kabla  ya kukamatwa .

Iran inadai kwamba Rigi amekuwa anaongoza mashambulio dhidi ya nchi  hiyo  kutokea Pakistan. 

Shirika la habari ,la Iran limemkariri waziri wa upelelezi  bwana Moslehi akisema kuwa Abdolmalek Rigi  alikamatwa  ndani ya ndege iliyokuwa inaelekea  Kyrgyzstan  kutokea Dubai.

Waziri Moslehi amesema  kukamatwa kwa kiongozi huyo  wa kundi  la wanaitikadi kali wa kisunni, ni kashfa  kubwa   kwa Dubai.Ameeleza kuwa  mkasa huo unaonyesha jinsi  Israel inavyozitumia Marekani  na nchi za Ulaya kwa lengo la kuligeuza eneo la nchi za kiarabu kuwa maficho ya  magaidi.

Iran imekuwa inamsaka Rigi  kwa miaka kadhaa ambae inadai ana uhusiano na idara za ujasusi za Pakistan, Uingereza na Marekani.

Abdomalik Rigi anadaiwa kufanya mashambulio katika jimbo la Sistan-Baluchistan  linalopakana na Afghanistan  na Pakistan, njia  kubwa ya  mihadarati.

Jimbo la Sistan Baluchistan ni maskani ya idadi kubwa  ya   wasunni na ni jiko la upinzani   dhidi ya watawala wa kishia wa Iran.

Kundi la Abdolmalik Rigi, Jundallah  lilidai kuwa lilifanya shambulio la kujitoa mhanga katika mji Pisheen ambapo   watu  42 waliuawa ikiwa pamoja na  walinzi saba wa mapinduzi  ya Iran  na viongozi  kadhaa wa makabila Shambulio hilo lilifanyika  mwezi oktoba mwaka  jana.

Kundi hilo pia lilidai kuwa lilifanya shambulio la bomu mwezi mei mwaka jana, kwenye msikiti  wa washia Amir al-Momenin katika mji wa   Zahedan nchini Iran.

Watu 20  waliuawa na hamsini walijeruhiwa.

Maafisa wa Iran wamesema Rigi mara  kwa mara  alikuwa anavuka mpaka kutoka Pakistan na kuingia Iran ili  kuongoza mashambulio katika  jimbo la Sistan- Baluchistan ndani  ya Iran.

Iran pia imemtia ndani Mohammed Ali Jafari nduguye    Abdolmalik  ambae  amewekwa katika orodha ya watu  wanaosubiri adhabu ya kifo.Abdolmaliki pia amesema   kundi la Jundallah lilipewa  amri   kutoka Marekani , za kufanya  mashambulio ndani ya Iran. Amesema kundi hilo  lilianzishwa  na linagharimiwa    na Marekani.

Mwandishi/Mtullya  Abdu/AFPE/RTRE/

Mhariri/Abdul-Rahman