1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

030408 Hu Jia Urteil

Aldenrath, Petra / Peking (RBB) 3 Aprili 2008

Safari ya mwenge wa Olimpiki huko China inaitwa "Safari ya amani". Lakini nchini China kwenyewe kuna mambo kadhaa ambayo yanazusha wasiwasi, hususan juu ya kazi za binadamu.

https://p.dw.com/p/DbVx
Hu Jua, mwanaharakati wa haki za binadamu wa ChinaPicha: picture-alliance/ dpa

Shirika la kimataifa linalotetea haki za bindamu, Amnesty International, limetoa taarifa kwamba muda huu mfupi kabla ya michezo ya Olimpiki kuanza, hali ya haki za binadamu ni mbaya sana. Mfano mwingine wa leo ni hukumu ya kifungo cha miaka mitatu na nusu aliyopewa mwanaharakati maarufu wa haki za binadamu wa China, Bw. Hu Jia. Maja Dreyer ana ripoti kamili.


Hu Jia mwenye umri wa miaka 34 ni mwanaharakati wa haki za wananchi na mazingira, mkosoaji wa serikali na muumini wa dini ya Kibuddha - na pia ni miongoni wa hao watu wenye maoni tofauti na huyataja wazi. Kwa muda kadhaa sasa, idara za usalama za China zinamwangalia mwanaharakati huyu kuwa ni mwenye kuleta hatari kwa usalama wa nchi hiyo ya kikomunisti, hususan baada ya Hu Jia alipofichua kashfa ya ugonjwa wa ukimwi ambayo serikali ilijaribu kuificha.


Hukumu ya kifungo cha miaka mitatu na nusu ambayo Hu Jia aliyopewa leo na mahakama ya Beijing ni kutokana na makala sita aliyoyachapisha katika mtandao wa Internet pamoja na mahojiano mawili aliyotoa kwa vyombo vya habari vya nje. Kulingana na mahakama, makala haya yanadhoofisha mamlaka ya serikali ya China.

Chinesischer Dissident Hu Jia zu dreieinhalb Jahren Haft verurteilt
Wakili Li Fangping akiongea nje ya mahakama mjini BeijingPicha: picture-alliance/ dpa


Wakili wa Hu Jia alikiri kuwa makala haya ni ya kuzikosoa sera za China lakini kwa njia ya amani. Anamshauri Hu Jia kukata rufaa ya hukumu, hususan kwa sababu ya afya yake. Hu Jia ana ugonjwa mbaya wa ini ambao inambidi apewe matibabu kila mara kwa mara. Wakili Li Fangping amesema: “Tunaweza kuomba aachiliwe huru akiwa chini ya adhabu ya kutofanya kosa akiwa nje tukitoa hoja ya hali yake mbaya ya afya. Hu Jia hajasema hata neno moja leo. Alisikiliza tu hukumu na hakusema chochote.”


Hu Jia alikamatwa mwishoni mwa mwaka ulipita, lakini kwa muda wa miaka miwili aliwekwa kwenye kizuizi cha nyumbani.


Mwezi wa Novemba mwaka uliopita, Hu Jia aliripoti mbele ya bunge la Ulaya akitumia mawasiliano ya video kupitia mtandao wa Internet na kuzungumzia hali ya haki za binadamu nchini mwake kabla ya michezo ya Olimpiki. Wadadisi wa mamabo wanaamini kuwa mazungumzo hayo ndiyo sababu ya kukamatwa kwake. Mwenyekiti wa bunge la Ulaya, Bw. Hans-Gert Pöttering anataka Hu Jia aachiliwe huru. Amesema: “Sisi kama wabunge wa Ulaya tunataka michezo hiyo ya Olimpiki ya mjini Beijing yawe na mafanikio. Lakini wakati huo huo tunataka haki za binadamu ziheshimiwe." Bw. Pöttering alieleza pia ama Hu Jia alizungumza na bunge la Ulaya kupitia mtandao wa Internet, basi hii inaenda sambamba na sheria za kimataifa. Lazima kuwepo mawasiliano huru ya kimataifa, alisema.


Hukumu hiyo dhidi ya Hu Jia ilikosolewa vikali na mashirika mbali mbali ya kutetea haki za binadamu pamoja na balozi wa Marekani nchini China.


Waziri mkuu wa China, Wen Jiabao alikanusha kwamba china iliongeza shinikizo dhidi ya wakosoaji wake kabla ya michezi ya Olimpiki na kwamba idadi kubwa zaidi ya watu walikamatwa.


Vilevile leo hii, kamati ya kimataifa ya michezo ya Olimpiki imekanusha mashtaka dhidi ya China kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu na ikasema kwamba ripoti zinazosema hivyo kama ile ya shirika la Amnesty International si za kweli.