1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano wa wanachama wa NATO Ugiriki na Uturuki wapamba moto

Zainab Aziz Mhariri: Iddi Ssessanga
22 Julai 2020

Uturuki imekanusha madai ya Ugiriki kwamba meli zake za utafiti wa mafuta na gesi zinavinjari kwenye eneo la mashariki mwa bahari ya Mediterania hilo limeongeza mvutano kati ya mataifa hayo mawili.

https://p.dw.com/p/3fgYJ
Türkei Istanbul | Bohrschiff "Yavuz"
Picha: Getty Images/AFP/B. Kilic

Uturuki ilitangaza mpango wa kupeleka meli zake za utafiti kwenye eneo la bahari ya Mediterenia ambalo ni la mzozo kati ya nchi hiyo na Ugiriki. Hatua hiyo imeongeza mivutano baina ya nchi hizo jirani. Kwa mujibu wa taarifa Uturuki imepuuza miito ya nchi za Ulaya juu ya  kuepusha mivutano. Hata hivyo wizara ya mambo ya nje ya Uturuki imerudia mwito wa nchi hiyo juu ya kufanyika mdahalo ili kuutatua mgogoro baina ya nchi mbili hizo ambazo ni wanachama wa mfungamano wa kijeshi wa NATO.

Waziri Mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis amesema hatua ya Uturuki ni changamoto kwa haki za nchi za  Ulaya kwenye mkutano na waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani heiko Maas.

Waziri Mkuu Mitsotakis amesema ikiwa Uturuki itaendelea katika mkondo huo, kuwekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya ndiyo itakuwa njia pekee ya kusonga mbele. Naye waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas anaefanya ziara nchini Ugiriki ametoa wito wa kuepuka vitendo vya uchokozi na badala yake kushiriki kikamilifu katika mchakato wa mazungumzo uliopangwa  kufanyika na Umoja wa Ulaya.

Waziri Mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis
Waziri Mkuu wa Ugiriki Kyriakos MitsotakisPicha: picture-alliance/AP Photo/P. Giannakouris

Ugiriki na Uturuki, ambao ni wanachama wa jumuiya ya kijeshi ya NATO wamekuwa wanazozana juu ya haki za kutafuta na kuchimba mafuta na gesi kwenye bahari ya Mediterania wakati ambapo Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya ziliendelea kuitupia lawama Uturuki kutokana na mipango yake ya kuendeleza  shughuli za uchimbaji wa mafuta na gesi kwenye sehemu ya bahari hiyo ambayo Ugiriki inadai kuwa ni yake.

Hata hivyo Uturuki imeilaumu Ugiriki kwa kujaribu kuitenga ili isinufaike na raslimali za mafuta na gesi zilizopo kwenye bahari za Aegean na Mediterania na imehoji kwamba mipaka ya bahari kwa ajili ya shughuli za biashara inapaswa kugawanywa baina ya nchi hizo mbili. Wakati huo huo televisheni ya serikali nchini Ugiriki imesema kuwa majeshi ya nchi hiyoyamewekwa katika hali ya tahadhari.

Vyanzo: AP/RTRE