1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano wa kamera za usalama Ujerumani

28 Desemba 2016

Shambulizi la kigaidi kwenye soko la Krismasi mjini Berlin lililosababisha vifo vya watu 12 na wengine kujeruhiwa vibaya limeibua mjadala mkali kuhusiana na uhalali wa kamera za usalama za video kwenye maeneo ya umma

https://p.dw.com/p/2UyHL
Symbolbild Videoüberwachung
Picha: imago/S. Schellhorn

Mwito huo wa kuongezwa kamera unasababisha majaji na wataalamu wa masuala ya data kuonya kuhusu hatua hiyo. 

Kuongezwa kwa idadi ya kamera za usalama kwenye maeneo ya umma hakutakuwa suluhu ya kuimarisha hali ya usalama, na badala yake zitaondoa uhuru wa raia, jaji mmoja kutoka taasisi ya majaji nchini hapa ameliambia shirika la habari la Ujerumani, Dpa. 

Washambuliaji wanaweza kulenga hata maeneo yenye ulinzi wa kamera za usalama za CCTV, ili kufanya uhalifu wao kuonekana wazi kwa umma, amesema mkuu wa taasisi ya kisheria, Jens Gnisa.

Wanasiasa kutoka maeneo kadhaa nchini Ujerumani wamesimamia upande huo wakipinga matumizi ya camera za CCTV katika kuwasaka wahusika. Wataalamu kutoka idara za data kutoka majimbo mbalimbali wameonyesha wasiwasi wao kuhusu hatua hiyo. Kamishna wa zamani wa masuala ya data, ambaye hakutaja jina lake, amekiambia kituo cha utangazaji cha RBB kwamba washambuliaji wa kujitoa muhanga hutaka kujionyesha kwa umma.  

Italien Anis Amri in Mailand
Picha inayomuonyesha Amri akiingia kituo cha kati cha treni mjini Milan.Picha: picture alliance/dpa/Italian Police

Anis Amri, raia wa Tunisia aliayeaminika kufanya shambulizi hilo la Berlin kwa kuingiza lori katikati ya soko la Krismasi lililokuwa limefurika watu, alifanikiwa kuitoroka mamlaka alipoukimbia mji huo baada ya shambulizi. Polisi iliwataka raia kuleta picha za shambulizi hilo ambazo zingeweza kusaidia katika uchunguzi.

Disemba 22, picha ya Amri ilionekana kwenye kamera za CCTV, mjini Lyon Ufaransa, na siku moja baadae alionekana mjini Milan, Italia ambako aliuwawa kwa kupigwa risasi na polisi. Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel alipozungumza baada ya kuuwawa kwa Amri alisema serikali itawajibika kuhakikisha usalama wa raia wake kwa namna yoyote.

Wizara ya mambo ya ndani imeitaka Berlin kuongeza kamera za CCTV, ingawa mamlaka za jiji hilo ambayo ni muunganiko wa vyama vitatu vya Social Democrats, SPD, chama cha kijani na cha mrengo wa kushoto cha Die Linke kwa pamoja wamesema wanajadili suala hilo. Watatoa mapendekezo yao mwezi ujao amesema msemaji wa tawala za ndani mjini Berlin kutoka chama cha SPD, Martin Pallgen. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Thomas de Maiziere amelitaka baraza la Seneti la jimbo kufikiria haraka msimamo wake.

Naibu mkuu wa moja ya vyama vikubwa vya polisi vya Ujerumani Ernst Walter ameiambia DW kwamba polisi wanajua bila ya kidhibiti cha picha hawawezi kumkatama mhalifu, na kutaka kuondolewa kwa mvutano kuhusu umuhimu wa vifaa hivyo kwa usalama.

Mwandishi: Lilian Mtono./ http://www.dw.com/en/berlin-under-pressure-to-enhance-video-surveillance/a-36923231
Mhariri: Grace Patricia Kabogo