1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano baina ya Israel na Marekani ?

Abdu Said Mtullya18 Machi 2010

Israel yapaswa kujihadhari, la sivyo itajitenga na jumuiya ya kimataifa.

https://p.dw.com/p/MVxy
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton.Picha: AP

Baada Israel kuamua kusonga mbele na ujenzi wa maakazi ya walowezi mashariki mwa Jerusalem,na hivyo kuikasarisha Marekani,sasa nchi hizo zinajaribu kutuliza mvutano uliotokea.

Hatahivyo Israel inapaswa kujihadhari la sivyo itajitenga na jumuiya ya kimataifa.Hayo anasema mwandishi wetu Rainer Sollich katika maoni yake.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Israel, makamu wa rais wa Marekani Joe Biden na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu-walizungumza kwa njia ya simu kwa muda mrefu, katika juhudi za kuuondoa mvutano baina ya nchi zao.Orodha ya wanasiasa waliotumia maneno makali dhidi ya Israel kutokana na uamuzi wake wa kujenga makaazi ya waloweti wa kiyahudi mashariki mwa mji wa Jerusalem ni ndefu katika kiwango ambacho siyo cha kawaida.

Waliotamka kuwa uamuzi wa Israel unaenda kinyume na sheria ni pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton .Na hata wanasiasa wa nchi za magharibi ambao hadi sasa wamekuwa wanaegemea sana katika upande wa Israel safari hii wametoa kauli kali dhidi ya nchi hiyo.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema uamuzi wa Israel ni kipingamizi kikubwa. Na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton alionyesha msimamo wake dhahiri kiasi kwamba wachunguzi walishaanza kuzungumzia juu ya kuwapo mgogoro wa kidiplomasia kati ya Marekani na Israel.

Ishara zilionyesha wazi. Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden alibezwa. Israel ilitangaza uamuzi juu ya ujenzi wa makaazi ya walowezi wakati mwanasiasa huyo akifanya ziara Mashariki ya Kati katika juhudi za kutafuta amani. Na baada ya wapalestina kuyasusia mazungumzo yaliyopangwa kufanyika, ikiwa ni ishara ya kupinga uamuzi wa Israel, Marekani iliahirisha ziara ya mjumbe wake wa Mashariki ya Kati George Mitchell. Hiyo ilitambulika kama ishara bayana kutoka Marekani ya kupinga hatua ya Israel.

Hatahivyo matukio hayo hana maana ya kubadilika kwa siasa ya msingi ya Marekani katika Mashariki ya Kati.

Marekani na Israel zina mtazamo mshabaha juu ya tishio la magaidi na waislamu wenye itikadi kali. Kati ya nchi hizo pana mfungamano wa ndani,kiutamaduni na kihisia.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton ametamka wazi kwamba Marekani na Israel zina mfungamano usiotetereka.Pia hakuna mtu mwenye mashaka juu ya mshikamano wa Kansela wa Ujerumani na Israel.Kutokana na sababu za kihistoria mshikamano huo ni sehemu ya siasa ya Ujerumani.

Lakini pamoja na hayo yote Israel inapaswa, kwa manufaa yake, ijihadhari, ili isijitenge na jumuiya ya kimataifa. Israel inahitaji kuungwa mkono kwa wote na washirika wake ili kuweza kufikia suluhisho na wapalestina. Mazungumzo ya kuleta amani na wapalestina yanapaswa kuanzishwa haraka na kwa ajili hiyo haitakuwa sawa kwa Israel kupitisha maamuzi yatakayoyafanya mazungumzo hayo yawe magumu.

Sera ya kupanuza mipaka na ya ujenzi wa makaazi ya walowezi, ni kinyume na sheria za kimataifa na vilevile ni hatua zinazorutubisha ugaidi miongoni mwa wapalestina.

Sera hizo zinaipa Israel usalama bandia. Usalama wa kweli kwa Israel utatokana na kuundwa kwa nchi ya wapalestina itakayoishi kwa amani na Israel.

Mwandishi/Sollich Rainer/ZA

Tafsiri/Mtullya Abdu.

Mhariri/Abdul-Rahman