1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mvutano bado kuhusu uhuru wa jimbo la Kosovo

Waziri mkuu wa Kosovo Agim Ceku ametoa mwito kwa viongozi wa Ulaya kuuepuka umoja wa mataifa na kuendelea na hatua za kuutambua uhuru wa Jimbo la kusini mwa Serbia licha ya pingamizi kutoka kwa Urusi na Serbia.

Waziri mkuu wa Kosovo Agim Ceku

Waziri mkuu wa Kosovo Agim Ceku

Matamshi hayo ya waziri mkuu wa Kosovo yamejitokeza wakati ambapo waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Bernard Kouchner yuko mjini Belgrade kukutana na viongozi wa Serbia licha ya kujitokeza mifano kwamba bara la Ulaya liko tayari kuutambua uhuru wa Kosovo bila ya kuunga mkono azimio la umoja wa mataifa.

Waziri mkuu wa Kosovo Agim Ceku amewaeleza waandishi wa habari mjini Brussels, Ubelgiji baada ya kukutana na mkuu wa sera za mambo ya nje wa umoja wa Ulaya Javier Solala kwamba anaona haitawezekana kufikia makubaliano katika baraza la usalama la umoja wa mataifa na kwamba ni ni lazima ukweli ukubalike kuwa baraza la usalama halina jibu la kila swali.

Bwana Ceku amesisitiza kuwa Kosovo iko tayari na inahitaji kuendelea mbele.

Ufaransa, Uingereza na Marekani zimependekeza mapumziko ya siku 120 kabla kuamuliwa hali ya baadae ya jimbo la Kosovo baada ya uamuzi wa Urusi ambayo ni mshirika wa Serbia kupinga vikali uhuru wa jimbo hilo la kusini chini ya usimamizi wa umoja wa mataifa.

Azimio la awali la umoja wa mataifa kuhusu Kosovo lilikataliwa na Urusi na Serbia na mazungumzo baina ya uongozi wa Kosovo na Serbia huenda yatafufuliwa hivi karibuni ili kujaribu tena kutafuta muafaka baina ya pande mbili hizi.

Rais George Bush wa Marekani, kwa upande wake anasema kuwa mwishowe utakuwa ni uhuru kwa eneo la Wakosovo milioni mbili wenye asili ya Kialbania.

Mazungumzo ya pande hizo mbili yaliyodumu kwa miezi kadhaa yalishindwa kufikia maelewano kutokana na Wakosovo wenye asili ya Kialbania kudai uhuru wao bila masharti yoyote huku Serbia ikisisitiza juu ya utamaduni na enzi yake ya kihistoria.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Bernard Kouchner katika mazungumzo yake leo na waziri wa mambo ya nje wa Serbia Vuk Jeremic mjini Belgrade amemueleza kuwa haitowezekana kwa Serbia kujiunga na umoja wa ulaya kabla ya kufikia makubaliano kuhusu Kosovo.

Kouchner pia atakutana na rais Boris Tadic wa Serbia na waziri mkuu Vojislav Kostunica kabla ya kuelekea katika mji wa Pristina hapo kesho katika juhudi za kuwashawishi viongozi wa Kosovo washiriki katika duru mpya ya mzungumzo.

Ufaransa inaunga mkono azimio la umoja wa mataifa la uhuru wa jimbo la Serbia lenye Waalbania wengi chini ya usimamizi wa umoja wa mataifa lakini Serbia inayoungwa mkono na Urusi inapinga vikali azimio hilo.

Balozi wa Marekani katika umoja wa mataifa Zalmay Khalilzad amesema kwamba Uingereza, Ufaransa na Marekani zimefikia makubaliano kuhusu masahihisho katika azimio la baraza la usalama la umoja wa mataifa na zinajdili swala hilo na Urusi.

Masahihisho hayo lakini hayahakikishi uhuru wa Kosovo.

Urusi imetishia kutumia kura ya turufu dhidi ya azimio lolote ambalo litakiuka matarajio ya mshirika wake Serbia.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com