1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muuwaji afikishwa mahakamani Oslo

25 Julai 2011

Anders Behring Breivik, anaetuhumiwa kuwauwa watu wasiopungua 93 anatazamiwa kufikishwa mahakamani hii leo mjini Oslo katika wakati ambapo nchi nzima ya Norway imejiinamia ikikumbuka unyama uliotokea.

https://p.dw.com/p/122rq
Wanorway waomboleza mauwaji ya kikatili ya Oslo na UtoyaPicha: dapd

Anders Behring Breivik ameshakiri yeye ndiye alioyeuwa lakini anakataa kubeba dhamana ya uhalifu wa mauwaji hayo ya kikatili kabisa kuwahi kushuhudiwa nchini Norway tangu vita vikuu vya pili vya dunia vilipomalizika.

Kijana huyo wa miaka 32 anatazamiwa kufikishwa mahakamani leo mchana kujibu masuala kuhusiana na mashambulio ya bomu yaliyotokea ijumaa iliyopita pamoja na mauwaji ya umati wa watu aliowafyetulia risasi-visa alivyoviandaa muda mrefu uliopita na kuvitekeleza bila ya kupepesa.

Mkuu wa Polisi Sveinung Sponheim anasema:

"Amekiri kwamba yeye ndie dhamana wa shambulio la bomu na mauwaji ya watu waliokuwepo katika kisiwa.Hakutoa sababu yoyote..lakini hiyo ni sehemu tu ya kuhojiwa kwake.."

Norwegen nach Terroranschlag Flash-Galerie
Waziri mkuu wa Norway Jens StoltenbergPicha: dapd

Wakili wa Andres Behring Breivik,Geir Lippestad amezungumzia matakwa mawili ya mteja wake:Kwanza anataka kesi hiyo iwe ya hadhara na pili aruhusiwe kuvaa kijeshi.

Lakini taarifa ya mahakama inasema kesi hiyo itasikilizwa kwa siri na mwendesha mashtaka ameshauri mtuhumiwa aendelee kushikiliwa rumande kwa angalao wiki nane.

Kwa mujibu wa polisi nchini Norway,huenda idadi ya wahanga wa mauwaji katika kisiwa cha Utoya,umbali wa kilomita 40 toka mji mkuu Oslo ikawa ndogo kuliko vile ilivyotajwa hapo awali.Hadi wakati huu tulio nao maafisa wa serikali wamekuwa wakizungumzia juu ya watu 86 waliopigwa risasi na kuuliwa katika kisiwa cha Utoya na saba waliopoteza maisha yao kufuatia shambulio la bomu dhidi ya jengo lenye ofisi za waziri mkuu Jens Stoltenberg mjini Oslo.

Majina na picha za wahanga huenda zikachapishwa muda mfupi ujao na waziri mkuu Jens Stoltenberg amewatolea mwito wa Norway wasalie kimya kwa dakika moja saa sita za mchana hii leo kote nchini humo.

Maafisa kaadhaa wa ngazi ya juu wa chama tawala cha Social Democratic wanahofiwa kuwa miongoni mwa waliouwawa.

Attentäter Norwegen Anders Behring Breivik
Anders Behring BreivikPicha: AP

Anders Behring Breivik alikuwa nusra amuuwe pia waziri mkuu wa zamani Gro Harlem Brundtland aliyekuwa miongoni mwa viongozi wa chama waliohudhuria kongamano la chama chao huko Utoya.Aliondoka muda mfupi tu kabla ya Behring Breivik kuwasili.

Mashambulio ya ijumaa yamechochea sauti kupazwa kudai adhabu ya kifo irejeshwe.Adhabu kali kabisa nchini Norway ni kifungo cha miaka 21 jela .

Behring Breivik amekiri kwamba amefanya mauwaji ya "kinyama" lakini anasema lengo lake ni kukomesha ukoloni wa kiislam barani Ulaya.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters,/AFP

Mhariri Yusuf Saumu