1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya mauaji ya Niels Högel yaongezeka

Lilian Mtono
29 Agosti 2017

Muuguzi Niels Högel alihukumiwa kifungo cha maisha 2015 kwa mauaji ya watu 30 katika hospitali mbili. Lakini uchunguzi wa karibuni waonyesha aliuwa watu zaidi ya 84.

https://p.dw.com/p/2j21s
Deutschland Mordprozess gegen Krankenpfleger
Picha: picture-alliance/dpa/I. Wagner

Baada ya miaka mitatu ya uchunguzi uliohusisha wagonjwa wote waliokuwa chini ya uangalizi wa muuguzi huyo Niels Högel, wachunguzi wamefichua Jumatatu kwamba muuguzi huyo wa zamani alihusika na vifo vingine 84, tofauti na ilivyofikiriwa hapo awali.

Högel ambaye tayari anatumikia vifungo viwili tofauti jela, alikutwa na makosa ya kuwachoma sindano wagonjwa waliokuwa wanapata matibabu ya magonjwa ya moyo katika hospitali zilizokuwa kwenye miji iliyoko magharibi mwa Ujerumani ya Oldenburg na Delmenhorst kati ya mwaka 1999 na 2005. Lengo lake lilikuwa ni kusimamisha mapigo ya moyo ama kusababisha mshituko wa moyo kabla ya kufanikiwa kuwafufua tena wagonjwa wake ili kuwafurahisha wafanyakazi wenzake.

Alihukumiwa kifungo cha hadi miaka saba na nusu mwaka 2008, kwa tuhuma za jaribio la kuua baada ya kugundulika akijaribu kumpa mgonjwa kiwango kikubwa cha dawa. Baadae mwaka 2015, alifungwa kifungo cha maisha jela baada ya kukutwa na hatia ya makosa sita ya mauaji, mawili ya kujaribu kuua na moja la kutumia nguvu baada ya jaribio lake kutofaulu. Hata hivyo waendesha mashitaka wametuhumu kwamba kuna uwezekano kuwa ameua watu wengi zaidi, lakini wamepunguza mashitaka ili kuyathibitisha kwa urahisi.

Klinikum Delmenhorst
Jengo la kliniki ya Delmenhorst, UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa/Ingo Wagner

Mwaka 2015 wakati kesi hiyo ikisikilizwa, Högel pia alikiri kwa mwanasaikolojia kuwa aliwaua watu 30 wakati akihudumu katika kliniki iliyopo Delmenhorst, kwa kuwadunga sindano ya dawa angalau wagonjwa 60. Mwaka jana, waendesha mashitaka walikisia idadi jumla ya vifo ilikuwa 43.

Hata hivyo, iwapo muuguzi huyo atapatikana na hatia ya vifo hivyo, idadi jumla ya vifo itapanda na kufikia angalu 90, na kumfanya kuwa mmoja wa muuaji wa watu wengi zaidi katika historia ya uhalifu nchini Ujerumani.

Kwa zaidi ya miaka mitatu, wachunguzi walisema walifukua na kuchunguza miili 134 ili kutathmini matibabu yaliyofanywa na Högel kwa mfumo wa damu mwilini, na hivyo kufanya idadi ya wanaohisiwa kuuawa na muuguzi huyo kufikia 84.

Mkuu wa polisi wa mji wa Olderburg, Johann Kühme, alisema kiwango cha matukio ya kihalifu yaliyofanywa na Högel "yamewaacha vinywa wazi". Na kama hilo halitoshi, amesema "tunatakiwa kutambua kwamba uhalisia wa mauaji hayo yaliyofanywa na Högel unawezekana mara nyingi ulikuwa wa kikatili."

Mkuu huyo wa polisi pia alizilaumu mamlaka za miji kwa kushindwa kuchukua hatua mara baada ya kufichuliwa kwa madai ya kuongezeka kwa karibu mara mbili idadi ya vifo katika kitengo cha wagonjwa mahatuti kwenye hospitali iliyopo mji wa Delmenhorst wakati ambapo Högel alikuwa akihudumu.

"Kama watu waliohusika wakati huo na hususani kwenye kliniki iliyoko Oldenburg, lakini baadae pia katika kliniki iliyopo Delmenhorst wasingesita kuziarifu mamlaka, kama waendesha mashitaka wa polisi, Högel angekamatwa mapema," amesema mkuu wa polisi wa mji wa Olderburg, Johann Kühme.

Madaktari wawili waandamizi wa zamani na mkuu wa kituo cha Delmenhorst pia wanakabiliwa na mashitaka ya mauaji wakihusishwa na vifo vya wagonjwa hao.

Kühme amesema mashitaka mapya dhidi ya Högel yanapangwa, kuanza kusikilizwa ama mwishoni mwa mwaka huu au mapema mwaka 2018. Hata hivyo, kwa kuwa tayari muuguzi huyo wa zamani anatumikia kifungo cha maisha jela, hukumu hiyo haitarejelewa kwa kuwa mfumo wa kisheria wa Ujerumani hauruhusu adhabu zinazofuatana.

Mwandishi: Lilian Mtono

Mhariri: Josephat Charo