1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muswada tete kupigiwa kura leo nchini Ufaransa.

22 Oktoba 2010

Vyama vya wafanyakazi vyaapa kuendelea na maandamano.

https://p.dw.com/p/Pl34
Waandamanaji wamevuruga shughuli katika viwanda 12 vya kusafishia mafuta.Picha: AP

Migomo na maandamano bado yanaendelea kutokota nchini Ufaransa huku vyama vya wafanyakazi vikiapa kutolegeza kamba.

Maafisa wa polisi nchini Ufaransa mapema leo walipambana kuondoa vizuizi vilivyowekwa kuziba barabara ya kuelekea katika kiwanda kikuu cha kusafishia mafuta yanayosambazwa katika mji wa Paris. Serikali imetoa amri ya dharura kuwataka raia wanaogoma kuondoka mara moja.

Viongozi wa vyama vya wafanyakazi waliwaambia waandishi wa habari mjini Paris kwamba serikali imewapa barua ya kuwaonya kutovuruga shughuli katika viwanda vya kusafishia mafuta. Barua hiyo hutolewa wakati ambapo athari ya migomo hutishia hali ya usalama na hutoa pendekezo la kufunguliwa mashtaka ikiwa kundi husika halitatii amri.

Frankreich Proteste Oktober 2010
Serikali imetoa amri ya kukamatwa kwa yeyote atakayevuruga shughuli katika viwanda vya mafuta.Picha: AP

Kwa miezi miwili Ufaransa imekuwa ikizongwa na msururu wa maandamano dhidi ya azimio la rais Nicolas Sarkozy kutaka kuongeza umri wa kustaafu kutoka miaka 60 hadi 62 ifikapo mwaka wa 2018 na miaka 67 kwa wafanyakazi watakaopata malipo kamili ya uzeeni.

Waziri wa mazingira na uchukuzi, Jean-Louis Borloo aliwaambia waandishi wa habari kwamba shughuli katika viwanda kumi na viwili vya kusafishia mafuta zimevurugwa kwa siku 11 zilizopita na kituo kimoja kati ya vitano vya kuuza mafuta hakina mafuta. Waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa, Brice Hortefeux akigusia suala la vurugu akisema Ufaransa halitakuwa taifa la wale wanaoiba, na kupora mali. Kwamba Ufaransa ni taifa la watu waaminifu wanaotaka kuishi kwa utulivu na ametizama kwamba kuna watu wengine wanaotaka kutumia mipaka yao kama uwanja wa vita na halitakubalika kabisa.

Baraza la Senate la Ufaransa linatarajiwa kupiga kura leo kuhusu muswada huo wa mabadiliko ya mfumo wa kustaafu na unaweza ukawa sheria kirasmi mapema wiki ijayo baada ya kuratibishwa na kamati maalum ya bunge. Ikiwa muswada huo utapitishwa kuwa sheria, itaanza kutumika mapema mwakani.

Kulingana na utafiti uliofanywa na taasisi ya BVA na uliyoonyeshwa na runinga ya Canal Plus nchini humo, asilimia 69 ya waliohojiwa wanaiunga mkono migomo inayoendelea. Hata hivyo asilimia 52 wanaipinga mbinu ya kuzuia viwanda vya kusafishia mafuta ambayo imesababisha kupungua kwa usambazaji wa mafuta na kuvuruga usafiri nchini humo.

Charles Foulard ambaye ni mkuu wa chama chenye nguvu cha wafanyakazi cha CGT katika sekta ya usafishaji wa mafuta alisema vizuizi hivyo havikunuia kuzua mtafaruku nchini humo bali ni njia ya kuitaka serikali iridhie kufanya mazungumzo. Vyama vya wafanyakazi vimeapa kuendelea na maandamano na vimepanga kuwa maandamano mengine tarehe 26 mwezi huu na tarehe 6 Novemba.

Mwandishi, Peter Moss /AFP/DPA/AP

Mhariri, Josephat Charo