1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mustakabal wa Pakistan kujadiliwa hii leo

Mwadzaya, Thelma22 Agosti 2008

Serikali ya muungano wa Pakistan inajiandaa kufanya mazungumzo muhimu hii leo yanayoazimia kujadilia mustakabal wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/F2sn
Nawaz Sharif Kiongozi wa chama cha Pakistan Muslim League-NPicha: picture-alliance/ dpa


Vyama vikuu viwili katika muungano huo Pakistan Peoples Party PPP kinachoongozwa na Asif Ali Zardari na chama cha Pakistan Muslim League PML-N cha Nawaz Sharif vinapanga kukutana hii leo kujadilia mustakabal wa nchi hiyo.Masuala nyeti ni mrithi wa wadhifa wa rais vilevile hatua ya kuwarejesha kazini majaji waliotimuliwa na Rais wa zamani wa Pakistan Pervez Musharraf.Bwana Musharraf aliamua kujiuzulu mwanzoni mwa wiki hii ili kukwepa mashtaka rasmi ya kikiuka katiba. Kiongozi wa chama cha Pakistan Muslim League Nawaz Sharif ametisha kujiondoa kwenye muungano huo endapo majaji hawatarejeshwa kazini.Kwa mujibu wa msemaji wa chama hicho Siddiqul Farooq mazungumzo ya leo yatakita zaidi katika suala la majaji hao waliotimuliwa.Taarifa za hivi punde zinaeleza kuwa viongozi hao wameafikiana kujadiliana suala hilo bungeni wiki ijayo.


Wakati huohuo Tume ya Uchaguzi ya Pakistan imetangaza kuwa uchaguzi wa rais unapangwa kufanyika tarehe 6 mwezi ujao wa Septemba.Hatua hiyo inaashiria juhudi za kudumisha ustawi nchini humo ili kufanikisha harakati za kupambana na wanamgambo.Jamii ya kimataifa inatiwa shaka na mivutano iliyoko kwenye muungano wa Pakistan hususana masuala hayo nyeti ya urithi wa rais na majaji kurejeshwa kazini.



Tume ya Uchaguzi ya Pakistan itapokea hati za uteuzi tarehe 26 mwezi huu wa Agosti na zitafanyiwa tathmini siku mbili baada ya hapo.Muungano wa Pakistan mpaka sasa bado haujaafikiana kuhusu mwakilishi wake.Hata hivyo chama cha PPP kinaripotiwa kupendekeza kiongozi wake Asif Ali Zardari ambaye ni mume wake marehemu Benazir Bhutto aliyeuawa Disemba iliyopita katika shambulio la bomu.Wapiga kura katika eneo la jimbo la kusini la Sindh ambako ndiyo ngome ya chama cha PPP wanaripotiwa kuidhinisha pendekezo hilo.Azimio hilo kadhalika limeridhiwa na vuguvugu la Muttahida Qaumi lililo na uwakilishi muhimu bungeni.

Chama mwenza katika muungano huo PPP-N kinachoongozwa na Nawaz Shariff bado kinaripotiwa kuridhia mgombea ambaye hana mafungamano ya kisiasa vilevile kutoka kwenye jimbo dogo.


Kwa upande mwingine wanamgambo wa Taliban wameripotiwa kuongeza nguvu ya mashambulizi yao.Watu 64 walipoteza maisha yao baada ya bomu kulipuka karibu na kiwanda kikubwa cha silaha siku ya Alhamisi.Shambulio hilo la kujitoa muhanga lilikuwa kubwa zaidi kutokea tangu Bwana Musharraf kujiuzulu siku ya Jumatatu.Wapiganaji hao wa Taliban wametisha kuendelea na mashambulizi endapo serikali ya Pakistan haitositisha kampeni yake ya kimataifa ya kuvamia ngome za wanamgambo kwenye eneo linalopakana na Afghanistan.Kwa mujibu wa Maulvi Omar msemaji wa Tehreek-e-Taliban ,tawi la kundi Taleban nchini Pakistan mashambulizi ya aina hiyo yatafanyika katika miji mingine nchini humo ili kupinga operesheni za kijeshi zinazowalenga.

Itakumbukwa kuwa Pakistan ni mwandani mkuu wa Marekani hususan katika vita dhidi ya ugaidi.

Matukio hayo yanauweka pabaya muungano huo wa Pakistan ambayo ni taifa pekee la kiislamu lililo na silaha za nuklia.

Duru za polisi zinaeleza kuwa mshukiwa mmoja kati ya watatu katika shambulio hilo la Alhamisi amekamatwa.Shambulio hilo lilisababisha pia takriban watu 70 kujeruhiwa vibaya.

Kulingana na afisa wa polisi wa ngazi za juu koti moja lililosheheni silaha za kulipuka lilipatikana kwenye msala katika msikiti mmoja ulio karibu na kiwanda hicho cha silaha.

Jeshi la Pakistan kwa upande wake linaeleza kuwa limewaua yapata watu 500 wengi wao wapiganaji kwenye eneo la Bajaur katika kipindi cha majuma mawili yaliyopita.Kiongozi mmoja wa ngazi za juu wa kundi la Al Qaeda Ayman al-Zawahri alikwepa shambulio la makombora lililofanyika hukohuko Bajaur yapata miaka miwili iliyopita.

Kiuchumi sarafu ya Pakistan ya rupee inaripotiwa kupungua nguvu kwa mara ya pili katika kipindi cha mwezi mmoja kufuatia misukosuko ya kisiasa inayoendelea pamoja na usalama duni nchini humo.

Kwa sasa rupee ina thamani ya 77.10 dhidi ya dola ya Marekani.

Benki Kuu nchini Pakistan imetangaza kuwa imepata hasara ya zaidi ya dola bilioni 6 katika kipindi cha miezi minane.Thamani ya sarafu ya rupee imepungua kwa asilimia 18 katika kipindi cha miezi minne kwasababu ya misukosuko hiyo.