1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Musharraf na hali ya hatari

10 Agosti 2007

Rais Musharraf wa Pakistan ameghairi azma yake ya kutangaza hali ya hatari nchini.

https://p.dw.com/p/CH9m

Uamuzi wa jamadari Musharaf-rais wa kijeshi wa Pakistan kutotangaza hali ya hatari nchini imekaribishwa kwa mikono miwili hii leo kwa kutolewa mwito wa kuitisha uchaguzi pamoja na kuimarisha mapambano dhidi ya wafuasi wenye siasa kali katika maeneo ya mpakani na Afghanistan.

Jamadari Musharaf anashinikizwa kila upande wakati huu ndani na nje ya Pakistan:Rais Bush wa Marekani jana alimtaka jamadari Musharaf kuitisha uchaguzi na apambane kwa nguvu zaidi na wafuasi wa Al Qaeda na watalibani wanaoitumia ardhi ya Pakistan .

Jamadari Musharaf jana aliamua kutotangaza hali ya hatari nchini baada ya kushauriana na washauri wake kwa muda wa siku 2 huku Pakistan ikikabili kile mawaziri wa hadhi ya juu serikalini walichokiita “kitisho tangu kutoka ndani hata nje”.

“Kumekuwapo miripuko kadhaa mabomu katika maeneo ya mpakani na Afghanistan.Pia majeshi yamehujumiwa .Kwahivyo, uwezekano wa kunadi hali ya hatari ulikuwapo.

Ingefaa pia nisistize kwamba hali ya hatari haikutangazwa ingawa tulizingatia uwezekano wa hatua hiyo.”

Alisema mmoja wa washauri wa rais Musharaf.

Wapinzani wa jamadari Musharaf wanajiuliza:

“Hatua gani ingelifuatia tangazo hilo?

Hii ndio ilioitia wasi wasi Marekani.

Wamekuwa wakimuungamkono dikteta wa kijeshi kwa kuwa tu akitumikia masilahi yao.”

Duru zilizoarifiwa ziliopo karibu na rais Musharaf zinasema kuwa uamuzi wake kukataa mashauri ya washirika wake wa kisiasa ya kutangaza hali ya hatari kumetokana na nia yake ya kuitisha uchaguzi uliopangwa mwakani.

Gazeti moja liitwalo THE NEWS limesema nia pekee ya rais Musharraf, kutangaza hali ya hatari ingelikuwa kutaka kuimarisha utawala wake unaoregarega wakati huu na likaongeza kuwa hakuna msingi wa kiuadilifu wa kusimamia uamuzi kama huo.

Gazeti hilo likaongeza zaidi na nanukulu,

“Uamuzi wa kutamngaza hali ya hatari nchini haungeweza kuhalalishwa juu ya misingi ya uadlifu,sheria au katiba na kwahivyo umngelichangia tu kuleta machafuko zaidi nchini.”

Jamadari Musharraf amekuwa akikumbana na misukosuko mingi karibuni pamoja nayo ghadhabu juu ya jaribio lake lililotiwa munda na Mahkama kumsimamisha kazi hakimu mkuu wa Pakistan-jaribio ambalo wanaomkosoa wanadai alifanya kutaka kuimarisha madaraka yake.

Malalamiko ya umma yaliofuatia jaribio hilo ,na yale juu ya hatua zake kali za kupambana na wafuasi wenye itikadi kali mpakani mwa Afghanistan na juhudi za wapinzani wake wa madaraka kurejea nchini kutoka uhamishoni nchi za nje kugombea uchaguzi kumeongeza vijinga vya moto katika chungu chake kinachotokota.