1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Musharraf awasili Saudi Arabia

Maja Dreyer20 Novemba 2007

Nchini Pakistan maelfu ya wakili na wanaharakati wa upinzani wameachiliwa wakati rais Perves Musharraf amewasili nchini Saudi Arabia, nchi ya uhamishoni mwa mpinzani wake Musharraf, Nawaz Sharif.

https://p.dw.com/p/CPeO
Je, Musharraf atakutana na mpinzani huyu Nawaz Sharif aliyeko uhamishani nchini Saudi Arabia?
Je, Musharraf atakutana na mpinzani huyu Nawaz Sharif aliyeko uhamishani nchini Saudi Arabia?Picha: AP

Rais Pervez Musharraf ambaye pia ni mkuu wa jeshi alikabiliwa na shinikizo kubwa la ndani na nje kubatilisha sheria ya hali ya hatari ambayo aliiwekea nchi mwake tarehe 3 mwezi huu pamoja na kudaiwa kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki utafanyika hapo Januari.


Kama kutoa ishara kuwa hali ya hatari itadhoofishwa, msemaji wa wizara ya ndani wa Pakistan aliarifu kwamba wafungwa wasiopungua 3400 wataachiliwa leo Jumanne na wengine 2000 wataachiliwa hivi karibuni.


Wakati huo huo, Musharraf alisafiri kuelekea Riyadh, Saudi Arabia, kwa madhumuni ya kufanya mazungumzo ya kisiasa na mfalmu Abdullah. Kuna tetesi kwamba katika ziara hiyo ya siku mbili Musharraf huenda atakutana na mpinzani wake, waziri mkuu wa zamani Nawaz Shariff ambaye anaishi uhamishoni nchini Saudi Arabia tangu mwaka 1999 baada ya kuondoshwa maradakani na Musharraf. Miezi miwili iliyopita, Sharif alitaka kurudi Pakistan lakini mara tu baada ya kufika kwenye uwanja wa ndege wa Islamabad alirudishwa Saudi Arabia. Sharif alitishia kwamba chama chake cha Muslim League kitasusia uchaguzi. Kulingana na ripoti kadhaa, Sharif alikanusha tetesi hizo juu ya mkutano kati yake na Musharraf kabla ya hati ya hatari haijafutwa.

Jana, tume ya uchaguzi ilitangaza kwamba uchaguzi utafanyika tarehe 8 Januari, lakini rais Musharraf bado hajasema hali ya hatari itaondoshwa lini. Vyama vingine vya upinzani kama kile cha Bibi Benazir Bhutto vinafikiria pia kususia uchaguzi huu kwa vile havitarajii uchaguzi kuwa huru na wa haki.


Mwendeshaji mkuu wa Pakistan, Malik Mohammed Qayyum alisema leo, ikiwa mahakama itaamua hivyo, Musharraf ataapishwa kama rais wa kiraia Ijumaa au Jumamosi wiki hii. Bw. Qayyum alisisitiza kuwa kabla ya hapo, Musharraf atajiuzulu kama mkuu wa jeshi. Jana mahakama hiyo ilifuta mashtaka dhidi ya uchaguzi wa Musharraf kuwa rais hapo Oktoba akiwa bado mkuu wa jeshi.


Kusini mwa Pakistan, katika mji wa bandari wa Karachi, polisi ilizuia maandamano ya waandishi wa habari kupinga vizuizi dhidi ya vyombo vya habari vilivyowekwa na raisi. Ripoti zinazotoka huko zinasema zaidi ya waandishi 150 walikamatwa na wengine walijerihuwa. Vyombo kadhaa vya habari vya Pakistan vilizuiliwa kutokana na sheria ya hali ya hatari.