1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Museveni ashinda muhula wa sita madarakani

Daniel Gakuba
16 Januari 2021

Yoweri Kaguta Museveni ametangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi wa rais uliofanyika nchini Uganda Alhamisi wiki hii, akipata asilimia 58.6 ya kura zote. Bobi Wine amekuja katika nafasi ya pili akiwa na asilimia 34.8.

https://p.dw.com/p/3o14q
Großbritannien London 2020 | Yoweri Museveni, Präsident Uganda
Yoweri Museveni, Rais wa UgandaPicha: Henry Nicholls/REUTERS

Kulingana na mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Uganda, Simon Mugenyi Byabakama, asilimia 57,22 ya Waganda takribani milioni 18 waliojisajili kupiga kura waliitikia zoezi hilo la Januari 14.

Soma zaidi: Bobi Wine: Jeshi limezingira makazi yangu, niko mashakani

Amesema Museveni amepata asilimia 58.6 ya kura zote, akifuatiwa na Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine aliyepata  asilimia 34.8.  Kati ya wagombea wengine 9 wa urais hakuna aliyefikisha hata asilimia tano.

Byabakama amewataka raia wa Uganda kubaki watulivu na kuyakubali matokeo ya uchaguzi, na kuhimiza wale wanaosherehekea ushindi kuheshimi masharti ya kujikinga na ugonjwa wa COVID-19.

Miaka 40 kileleni mwa siasa za Uganda

Museveni aliyeingia madarakani mwaka 1986 baada ya kundi la waasi aliloliongoza kuyashinda majeshi ya serikali, akimaliza muhula huu atakuwa ameiongoza Uganda kwa miaka 40, na kuwa miongoni mwa marais waliodumu mamlakani kwa muda mrefu zaidi barani Afrika.

Uganda Wahl Robert Kyagulanyi Bobi Wine
Robert Kyagulanyi Bobi Wine, amekuja katika nafasi ya piliPicha: Sumy Sadruni/AFP/Getty Images

Wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi ikiyatangaza matokeo hayo mchana Jumamosi, makaazi ya Bobi Wine yaliyoko nje kidogo ya mji mkuu, Kampala yalikuwa yamezingirwa na wanajeshi. Ingawa chama chake kinasema hali hiyo ni kama kumweka katika kifungo cha nyumbani, serikali inadai ni katika juhudi za kuhakikisha usalama wake.

Soma zaidiMaoni: Uchaguzi wa Uganda ni fursa iliyopotea

Uchaguzi huu ulifanyika baada ya kutokea ghasia mbaya zaidi kuundama uchaguzi wa Uganda, ambapo watu 54 waliuawa, viongozi kadhaa wa upinzani kukamatwa na vyombo vya habari kufungiwa matangazo.

Wakati serikali ikisema uchaguzi ulifanyika katika mazingira salama, Boni Wine amesema ulijaa visa vya wizi wa kura na vurugu, akidai katika baadhi ya vituo mawakala wake walipigwa na kufukuzwa wasiweze kufuatilia kilichokuwa kikiendelea.

Bobi Wine ayapinga matokeo

Hapo jana alisema ''chochote kinachotangazwa ni upuuzi mtupu, na tunakikataa na kujitenga nacho.''

Uganda l Unruhen im November während der Kampagne von Kyagulanyi
Uchaguzi huu wa Uganda ulikumbwa na visa vingi vya vuruguPicha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Msemaji wa chama chake cha National Unity Platform (NUP) Joel Ssenyonyi, amsema hawawezi kuondoa uwezekano wa wafuasi wao kupinga matokeo yaliyotangazwa.

''Watu wana hasira kwa sababu kura zao zimeibiwa,'' amesema Ssenyonyi, na kuongeza kuwa yeye na Bobi Wine hawana haja ya kuwaelekeza namna ya kukasirika. ''Hata hatuwezi kuwadhibiti'', ameongeza.

Soma zaidi: Museveni aongoza matokeo ya awali nchini Uganda

Mwanadiplomasia mwandamizi wa Marekani barani Afrika Tobor Nagy amewataka wadau wote katika uchaguzi wa Uganda kujizuia kufanya vurugu, na kutaka mawasiliano ya intaneti na mitandao ya kijamii kufunguliwa. Mawasiliano hayo yamezimwa nchini Uganda kwa muda wa siku nne zilizopita.

Msemaji wa serikali mjini Kampala, Ofwono Opondo amesema intaneti ilizuiliwa ili kuepusha matumizi yake mabaya, yakiwemo kueneza taarifa za uongo kwa lengo la kuhujumu uhalali wa mchakato wa uchaguzi.

Vyanzo: afpe, dpae