1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mursi rais mpya wa Misri

24 Juni 2012

Mgombea wa Udugu wa Kiislamu nchini Misri, Mohammed Mursi, ameshinda urais wa nchi hiyo akiwa rais wa kwanza wa kuchaguliwa wa taifa hilo la Afrika ya Kaskazini, akishinda kwa asilimia 51.7 ya kura zote.

https://p.dw.com/p/15Kex
Mohammed Mursi.
Mohammed Mursi.Picha: Reuters

Maelfu ya wafuasi wake wanaendelea kushangiria kwenye uwanja maarufu wa Tahrir, ambako wamekusanyika tangu juzi kushinikiza kutangazwa kwa matokeo. Mursi, mhadhiri wa chuo kikuu amemshinda waziri mkuu wa zamani wa enzi za Hosni Mubarak, Ahmed Shafiq, ambaye hapo Alhamis wafuasi wake walitangaza kuwa ndiye mshindi.

Mursi sasa anakabiliwa na kazi ngumu ya kupatanisha tafauti za kimtazamo na kimadaraka kati ya vyama vinavyofuata siasa za Kiislamu, jeshi na makundi mengine nchini Misri.

Msemaji wa timu ya kampeni ya Mursi, Jihad al-Haddad, amekiambia kituo cha televisheni cha al-Jazeera, kwamba Mursi angelilihutubia taifa muda wowote kuelezea mpango wake wa uongozi.

Usalama waimarishwa

Vikosi vya ulinzi nchini Misri vilikuwa katika hali ya tahadhari wakati kukiwa na hofu kubwa ya kuzuka kwa ghasia katika dakika za mwisho kabla ya Tume ya Uchaguzi wa Taifa kutangaza mshindi wa duru ya pili ya uchaguzi wa wiki iliyopita kati ya Mursi na Shafiq.

Kura nchini Misri.
Kura nchini Misri.Picha: dapd

Jengo la Wizara ya Habari lilikuwa imezingirwa na polisi na wanajeshi. Hata kabla ya matokeo ya leo kutangazwa rasmi, tayari Mursi alikuwa ameshajitangaza kuwa mshindi wa kuchukuwa nafasi ya Mubarak aliyepinduliwa Februari 2011.

Kuelekea kutangazwa kwa matokeo haya, kulikuwa na khofu kubwa kwamba wafuasi wake wangelifanya vurugu iwapo ushindi huo ungelikwenda kwa Shafiq, jenerali wa zamani katika jeshi la Misri na rafiki wa Mubarak.

Wanajeshi wachache walionekana mitaani lakini maafisa wa usalama wamesema walikuwa tayari kukabiliana na vurugu hizo. Watumishi wa serikali walioko karibu na uwanja wa Tahrir ambapo maelfu ya wafuasi wa Udugu wa Kiislamu walikusanyika kwenye uwanja huo walitakiwa kurudi nyumbani.

Mitaa katikati ya mji mkuu wa Cairo ilikuwa haina watu kabisa, maduka yalifungwa na watu walibakia majumbani wakisubiri kwa hamu kubwa matokeo hayo.

Mgogoro wa madaraka

Licha ya matokeo hayo ni ya kihistoria huko Mashariki ya Kati lakini hayatomaliza mapambano ya kuwania madaraka kati ya jeshi, Waislamu wa itikadi kali na watu wa makundi mengine juu ya mustakbali wa Misri.

Wafuasi wa Mursi.
Wafuasi wa Mursi.Picha: picture-alliance/dpa

Chama cha Udugu wa Kiislamu na wanaharakati wa kiliberali ambao walimwagika mitaani mwaka jana kupinga utawala wa Mubarak walikuwa wakitarajiwa kuchemka kwa hasira ingelikuwa tume ya uchaguzi imemtangaza Shafiq kuwa rais mpya wa Misri.

Kama vile ilivyokuwa kwa Mubarak kila rais nchini Misri kwa miongo sita amekuwa akitokea jeshini. Shafiq alihudumu kama kamanda wa jeshi la anga, nafasi iliyowahi pia kutumikiwa na Mubarak.

Wamisri wengi na mamilioni ya watu huko Mashariki ya Kati wangeliuona ushindi wa Shafiq kama pigo la kifo kwa uasi wa Majira ya Machipuko katika ulimwengu wa nchi za Kiarabu licha ya hakikisho lake kwamba alikuwa pia anataka kuunda serikali itakayojumuisha pande zote.

Rais wa mwanzo wa kiraia na kutoka chama cha Kiislamu

Kwa Misri kupata rais wa itikadi kali za Kiislamu ni historia kubwa kwa Mashariki ya Kati jambo ambalo lilikua haliwaziki miezi 18 iliopita.

Ahmed Shafiq
Ahmed ShafiqPicha: picture-alliance/dpa

Mursi mwenye umri wa miaka 60, mhandisi aliyepata elimu yake nchini Marekani na mfungwa wa kisiasa wakati wa utawala wa Mubarak, alijitangazia ushindi muda mchache baada ya kumalizika kwa uchaguzi Jumapili iliopita hatua ambayo ililaaniwa na majenerali wanaotawala Misri.

Rais huyo mpya hatokuwa na madaraka makubwa kama yale waliokuwa wakiyategemea wagombea wa urais, wakati wa duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais hapo mwezi wa Mei wakati jeshi lilipoahidi kurudisha utawala wa kiraia hapo tarehe Mosi mwezi wa Julai.

Baraza la Kijeshi linalotawala Misri ambalo lilimuweka kando Mubarak hapo mwaka 2011 ili kuwatuliza waandamanaji waliokuwa mitaani limeondowa madaraka mengi ya urais na kulivunja bunge lililokuwa likiongozwa na Chama cha Udugu wa Kiislamu ambalo lilichaguliwa hapo mwezi wa Januari.

Mwandishi: Mohamed Dahman/RTR
Mhariri: Mohamed Khelef