1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mume Nguvuze !

24 Oktoba 2011

Timu mbalimbali zinashuka uwanjani katika mashindano ya kuyawania mataji ya Ujerumani na Uingereza

https://p.dw.com/p/12y1C
Nani ndiye atakaye kuwa mshindi?Picha: picture-alliance/Sven Simon

Timu ya Dynamo Dresden inatarajia kuzusha udhia mwingine kwa kunyakua ushindi katika raundi ya pili ya mashindano hayo hapo kesho, wakati timu hiyo iliopo kwenye daraja la pili itakapoteremka uwanjani dhidi ya mabingwa wa msimu uliopita wa ligi ya Bundesliga, Borussia Dortmund.

Champions League Gruppe E Olympiakos Piräus gegen Borussia Dortmund
Kocha Jurgen Klopp wa Borussia DortmundPicha: dapd

Katika raundi ya kwanza Dresden ilijizatiti na kuifunga timu ya aliyekuwa kapteni wa timu ya taifa, Michael Ballack, Bayer Leverkusen, mabao 4-3 katika muda wa ziada.

Na ndipo walipoipata nafasi ya hapo kesho katika mechi ya marudio watakaposafiri hadi kwa mabingwa Dortmund.

Mabingwa Dortmund kwa upande wao, walijinyoosha misuli wakijitayarisha kwa mpambano wa hapo kesho kwa kuchuana na Köln mwishoni mwa juma na kufanikiwa ushindi wa mabao 5 -0 katika ligi ya Bundesliga na mfungaji wa Poland Robert Lewandowski aliyafunga mawili na kufanya kuwa mabao 7 aliyofunga katika mechi 10 za ligi msimu huu.

Licha ya ushindi huo, nahodha wa Dortmund Sebastian Kehl, ameeleza kuwa timu yake haitopuuza uwezo wa Dresden hapo kesho. Katika mechi za ligi ya daraja la kwanza, Hoffenheim inaikaribisha Köln hapo kesho huku nayo Hannover inaikaribisha Mainz siku ya Jumatano.

Timu nyingine zitakazoteremka uwanjani hapo kesho katika mashindano hayo ni pamoja na RasenBallsport Leipzig dhidi ya FC Augsburg, Heidenheim dhidi ya Borussia Monchengladbach, Fortuna Dusseldorf dhidi ya 1860 Munich, Eintracht Trier dhidi ya Hamburg, na Hoffenheim dhidi ya Köln.

DFB-Pokalfinale 2011 MSV Duisburg - FC Schalke 04
Washindi Schalke 04Picha: AP

Katika mechi nyingine, washikilia kombe hilo la Ujerumani, Schalke 04, wanakaribishwa siku ya Jumatano na timu ya divisheni ya pili, Karlsruhe huku nayo timu inayooongoza kwenye Bundesliga, Bayern Munich inaikaribisha Ingolstadt 04, ambayo pia ipo katika divisheni ya pili, katika uwanja mkuu mjini Munich, Allianz Arena.

Kombe la Carling

Ama katika mashindano ya kuliwania kombe la Uingereza, baada ya kichapo ilichopokea hapo jana, ambalo bado ndiyo gumzo mitaani, sasa timu ya Manchester United, itajaribu kujikukuta vumbi hapo kesho dhidi ya timu ya Aldershot katika mashindano ya kuliwania kombe hilo, maarufu lijulikanalo kama Carling Cup.

Manchester United vs. Chelsea
Picha: dapd

Manchester United inasafiri kuelekea Hampshire saa 48 baada ya kuadhibiwa kwa mabao 6-1 na timu jirani hasimu, Manchester City, uwanjani Old Trafford, huku kocha Alex Ferguson akiwa na hamu kubwa ya kuondosha athari ya adhabu hiyo ya hapo jana haraka iwezekanavyo.

Kocha wa timu ya Aldershot Dean Holdsworth anatarajia kuwa kikosi chake kitaweza kujikakamua kinapojitayarisha kukutana na mashetani hao wekundu.

Champions-League-Vorschau Manchester gegen Schalke
Sir Alex FergusonPicha: AP

Huenda Ferguson akafanya mabadiliko katika kikosi cha hapo kesho, baada ya hapo awali Man U kuifunga Leeds katika raundi ya awali na huenda Ferguson, akawajumuisha Ji Sung Park, Ryan Giggs, Dimitar Berbatov, na Michael Owen dhidi ya AlderShot.

Katika mechi nyingine washikilia mizinga Arsenal, wanakabiliana na Bolton uwanjani Emirates, huku kikosi cha Arsene Wenger, kikitafuta ushindi wake wa 7 katika mechi nane ambazo imecheza mpaka sasa.

Bolton walifungwa 3-0 na Arsenal katika mpambano wa ligi hiyo mwezi uliopita na Kocha wa timu hiyo, Owen Coyle, anabidi awashinikize wachezaji wake kuwajibika baada ya kufungwa tena katika ligi hiyo na Sunderland mwishoni mwa juma.

Siku ya Jumatano, washindi wa hapo jana, katika ligi ya Uingereza, Manchester City, watakipumzisha kikosi cha kwanza dhidi ya Wolves, huku kwengineko, Everton wanaonana na Chelsea uwanjani Goodison Park.

Liverpool inasafiri hadi Stoke City, wakilenga kulipiza kisasi cha kufungwa bao 1-0.

Blackburn nayo inaonana na Newcastle.

Mwandishi: Maryam Abdalla/Rtre/Afpe/Dpae/
Mhariri:Josephat Charo