1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mugabe aonya dhidi ya kupandisha bei bidhaa

27 Juni 2007

Serikali ya rais Robert Mugabe wa Zimbabwe imetishia kuwa itazitaifisha kampuni zinazojihusisha na kuongeza bei za bidhaa kiholela.

https://p.dw.com/p/CHkO
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe
Rais Robert Mugabe wa ZimbabwePicha: AP

Rais Robert Mugabe ameuita huo kuwa ni mchezo mchafu ijapokuwa taifa hilo la kusini mwa Afrika limekumbwa na ongezeko kubwa la bei za bidhaa katika nyakati za hivi karibuni.

Katika hotuba yake kupitia redio na televisheni za taifa wakati alipohudhuria mazishi ya kamanda wa jeshi la Zimbabwe rais Mugabe alionya kuwa siku ya majuto itafika ambapo wafanyabiashara wote wanao kiuka mwito wake wa kupunguza bei za bidhaa watanyang’anywa biashara zao.

Huku akishangiliwa na maelfu ya raia kiongozi huyo hakusita pia kutishia kutwaa migodi ambayo ameilaumu kwa kuendelea kuficha pesa za kigeni kwa njia zisizo halali kupitia mfumo mgumu wa kubadilisha fedha.

Ukaguzi wa ghafla uliofanyika leo hii mjini Harare umegundua kuwa bidhaa kadhaa muhimu zimetoweka kutoka madukani.

Bidhaa kama vile mkate , mafuta ya kupikia, unga na maziwa zimepotea kwani hizo ni miongoni mwa bidhaa ambazo rais Mugabe aliagiza zipunguzwe bei.

Rais Mugabe pia aliuambia umati uliofika mazikoni wengi wao wakiwa ni askari kuhusu kung’atuka madarakani leo hii kwa aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair.

Amesema kuwa ana matarajio kwamba mrithi wake atazingatia hali ya Zimbabwe na sera za kale za Uingereza kwa lengo la kurekebisha sera hizo.

Rais Robert Mugabe anamlaumu waziri mkuu wa Uingereza anaeondoka Tony Blair na utawala wa zamani wa nchi hiyo kwa mashaka ya kiuchumi na kisiasa yanayoikumba Zimbabwe kwa sasa.

Zimabwe iliyotawaliwa na Uingereza tangu uhuru wake hapo mwaka 1980 inaongozwa na rais Robert Mugabe ambae utawala wake umekuwa daima ukikosolewa na aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair.

Serikali ya Zimbabwe inaulaumu utawala wa bwana Blair kwa kuchochea vikwazo vyote vinavyomkabili rais Mugabe na wapambe wake vikiwa ni pamoja na vikwazo vya kusafiri na kutaifishwa akaunti za benki kufuatia madai kwamba utawala wake ulihusika na wizi wa kura katika uchaguzi wa mwaka 2002.

Serikali ya rais Robert Mugabe inalaumiwa kwa hali ngumu inayowakabili raia ya kuongezeka kwa bei za bidhaa mara kwa mara nchini Zimbabwe.

Wafanyakazi wengi nchini humo wanapata kiwango cha chini sana cha mishahara ambacho hakiwezi kumudu mahitaji ya kimsingi ya kila siku.

Wachambuzi wa maswala ya kisiasa wanasema kwamba tishio hilo la serikali ya rais Mugabe la kutaifisha makampuni yakiwemo mabenki ya kigeni na shughuli za kusimamia migodi huenda likazidisha hali mbaya ya kiuchumi ya Zimbabwe.