1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mugabe ahimizwa kufanya mabadiliko ya kidemokrasia

Admin.WagnerD13 Juni 2011

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ameelezea kuridhishwa kwake na matokeo ya mkutano mkuu wa kikanda wa Jumuia ya maendeleo ya nchi zilizo kusini mwa Afrika SADC.

https://p.dw.com/p/11ZMP
Rais wa Zimbabwe Robert MugabePicha: AP

Mkutano huo uliofanyika jana nchini Afrika Kusini umemtaka Mugabe afanye mabadiliko ya kidemokrasia kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.

Muda mfupi baada ya kuwasili nchini Zimbabwe, rais Mugabe aliwaambia waandishi wa habari kwamba "Mkutano Umekwenda vizuri". Lakini kubwa lililosistitwa katika mkutano huo ni kufanyika marekebisho kabla ya wananchi wa Zimbabwe kushiriki uchaguzi mkuu.

Katika mkutano wake huo na waandishi habari, Rais Mugabe amemsifu msimamizi wa mkutano huo wa SADC, ambea ni Rais Jacob Zuma wa Afrika kusini, kwamba ametoa ripoti nzuri kuhusu mpango wa kugawana madaraka na hasimu wake wa muda mrefu, waziri mkuu, Morgan Tsvanfgirai.

Schweiz Wirtschaft Weltwirtschaftsforum in Davos Südafrika Jacob Zuma
Rais wa Afrika Kusini Jacob ZumaPicha: dapd

Rais Mugabe alisema, Zuma amedhirisha kwamba juhudi za pamoja za makubaliano ya kisiasa ya kimataifa zimefanikiwa na kinachotakiwa sasa ni muongozo wa kidemokrasia kuelekea uchaguzi mkuu.

Chama Tsvangirai, Movement for Democratic Change ( MDC), pia kimeyakaribisha matokeo ya mkutano wa SADC wa Johannesburg.

Katibu aneshughulikia mahusiano ya kimataifa wa MDC, James Temba, aliliambia gazeti mmoja nchini Afrika Kusini muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano huo kwamba wamefurahishwa na yaliyofikiwa katika mkunato huo.

Wakati mkutano huo umekubali kuyapokea mapendekezo ya muongozo wa mabadiliko ya kikatiba na uchaguzi, viongozi wamerudisha uamuzi huo katika mkutano mwengine wa SADC unaotarajiwa kufanyika mwezi Agosti.

Katika mkutano huo, viongozi kutoka mataifa 15 ya jumuiya hiyo ya SADC, walimtaka Rais Mubage na Waziri mkuu Tsvangirai kuongeza kasi ya kutekeleza makubaliano ya mgawanyo wa madaraka, ambayo yamewaunganisha pamoja katika serikali ya mseto iliyoundwa mwaka 2009.

Katika hatua nyingine mkutano huo wa SADC umeidhinisha muongozo wa kuelekea uchaguzi mkuu kwa nchi ya Madagascar kwa kumtaka Rais Andry Rajoelina kumruhusu rais aliendolewa madarakani ambae kwa hivi sasa anaishi uhamishoni, Mark Ravalomanana arejee nchini humo.

Rais huyo wa zamani alikataa kutia saini mpango wa kurejea nchini humo kwa mashariti ya kutaka kuwepo kwanza mazingira mazuri ya kisiasa na usalama kwa upande wake.

Lakini viongozi hao wa nchi 15 za Jumuiya hiyo ya Maendeleo ya nchi zilizo kusini mwa Afrika(SADC) ambao wamekuwa wakijaribu kusuruhusha mgogoro huo uliyomtoa madarakani Ravalomanana miaka miwili iliyopita wlisema mpango huo utapaswa kubadilika. Na kuitaka serikali ya Rajoelina kuridhia kiongozi huyo kurejea Madagascar kabla ya uchaguzi ujao.

Madascar ilisimamishwa uwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi zilizo kusini mwa Afrika-SADC- pamoja na Umoja wa Afrika tangu kuondolewa madarakani kwa Ravalomanana. Aidha Umoja wa Ulaya ulisimamisha msaada wa fedha wa kiasi cha euro milioni 600 kutokana na mkwamo wa kisiasa.

Mwandishi: Sudi Mnette//AFP

Mhariri: Miraji Othman