1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mugabe achangia Umoja wa Afrika dola milioni moja

Isaac Gamba
4 Julai 2017

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe amesema anachangia dola milioni moja kwenye Umoja wa Afrika akilenga kuonyesha mfano kwa nchi za Afrika ili kufadhili shughuli za Umoja huo na kuachana na misaada kutoka kwa wafadhili.

https://p.dw.com/p/2ft1o
29th African Union Summit
Picha: African Union Summit picture alliance / AA

Kwa miaka kadhaa sasa karibu asilimia 60 ya bajeti ya  matumizi ya Umoja wa Afrika imekuwa ikifadhiliwa na wafadhili ikiwa ni pamoja na Umoja wa Ulaya, Benki ya Dunia na mataifa mengine tajiri nje ya bara hilo.

Rais Robert Mugabe ambaye yuko madarakani tangu Zimbabwe ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Uingereza mwaka 1980, amesema kutegemea  msaada kutoka kwa wafadhili kunasababisha mataifa makubwa kuingilia masuala ya ndani ya  Umoja wa Afrika. 

Rais  Mugabe ambaye kwasasa ana umri wa miaka 93 amesema alilazimika kuuza mifugo yake 300 mwezi Mei ili kutimiza ahadi ya miaka miwili iliyopita.

Akikaririwa na televisheni ya  taifa ya Zimbabwe Rais Mugabe amesema  Afrika inapaswa kufadhili mipango yake wenyewe na kuwa taasisi kama ya AU haipaswi kutegemea pekee misaada kutoka kwa wafadhili.

Bajeti ya Umoja wa Afrika kwa mwaka  wa 2017   ni Dola milioni 782 ikipanda kutoka Dola milioni 416 mwaka jana.  Viongozi  wa Umoja huo mwaka jana walikubaliana kimsingi kutoza asilimia 0.2 katika mauzo ya nje ya  bidhaa kutoka barani humo ili kufadhili shughuli za Umoja huo.

Zimbabwe ambayo uchumi wake uliathiriwa na ukame uliolikumba taifa hilo mwaka jana haijaweka bayana mchango wake kwenye Umoja wa Afrika.

Mataifa matano barani humo yanayo ongoza kuchangia kwenye Umoja wa Afrika ni Algeria, Misri, Libya, Nigeria na Afrika Kusini.

AU yatakiwa kuzisaidia nchi zinazokabiliwa na njaa

Moussa Faki Mahamat
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki MahamatPicha: picture alliance/dpa/G.Onorati

Wakati huohuo Mwenyekiti wa Kamisheni ya  Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahmat hapo jana amezikusoa nchi wanachama wa Umoja huo kwa kushindwa kuonesha mshikamano kwa nchi zinazokabiliwa na janga la njaa barani humo.

Faki ambaye alikuwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Chad kabla ya kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo mwezi Januari amesema hawezi kuficha hisia zake kuhusiana na jinsi anavyoguswa na hali ya ukimya  uliopo kutokana na mataifa ya Afrika kushindwa kuchukua hatua katika kuzisaidia nchi zinazo kabiliwa na njaa barani humo.

Kuchaguliwa kwa Faki kulikuja siku kadhaa baada ya Umoja wa Mataifa  kusema ulimwengu unakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kibinadamu tangu kumalizika kwa vita ya pili ya dunia huku kiasi ya watu milioni 20 wakikabiliwa na utapia mlo pamoja na njaa nchini Yemen, Somalia, Sudan Kusini na Nigeria.

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika safari hii umejikita katika ajenda ya jinsi gani ya kuweza kufanya mageuzi ndani ya umoja huo pamoja na kuuwezesha kuto tegemea  ufadhili kutoka nje.

Wakati huohuo  Djibouti itautaka Umoja wa Afrika kusaidia katika kutatua mgogoro wa muda mrefu wa mpaka kati yake na Eritrea hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nje wa taifa hilo la pembe ya Afrika Mohamoud Ali Youssouf  alipozungumza na shirika la habari la AFP.

Vikosi vya jeshi la Qatari ambavyo vilikuwa vinaweka doria katika mpaka wa nchi hizo mbili viliodolewa mwezi uliopita baada ya Djibouti na Eritrea kuungana na Saudi Arabia wakati nchi hiyo ilipovunja uhusiano na Qatari kuhusiana na madai  ya Qatari kuunga mkono makundi ya kiisilamu yenye itikadi kali.

Mwandishi: Isaac Gamba/ AFPE

Mhariri      :Yusuf Saumu