1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muda wa kusimamisha mapigano Syria wamalizika

10 Aprili 2012

Kuanzia leo saa 11 alfajiri, umemalizika ule muda wa kuweka chini silaha nchini Syria, kwa mujibu wa mpango wa mjumbe maalum Kofi Annan.

https://p.dw.com/p/14aDY
Maandamano nchini Syria
Maandamano nchini SyriaPicha: Reuters

Idadi ya watu wanaokufa Syria inazidi kuongezeka licha ya kwamba siku ya kusitisha mapigano imefika. Katika muda wa saa 24 zilizopita watu zaidi ya 155 waliuawa ikiwa pamoja na askari 12 wa serikali. Mapigano makali zaidi yameripotiwa katika maeneo ya Homs, Aleppo na Daraa.

Leo hii waziri wa mambo ya nchi za nje wa Syria, Walid Moualem, amefanya mazungumzo na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov. Lavrov ameitaka Syria kuonyesha utayari wa kuufuata mpango wa amani uliopendekezwa na Kofi Annan. Waziri huyo alisema pia kwamba mataifa mengine yanapaswa kutumia ushawishi wao kuyahimiza makundi ya wapiganaji wa upande wa upinzani nchini Syria kuacha mapigano mara moja. Walid Moualem ameeleza kwamba serikali ya Syria tayari imeanza kuondoa wanajeshi katika baadhi ya miji ya nchi hiyo.

Walid Moualem katika mazungumzo na Sergei Lavrov
Walid Moualem katika mazungumzo na Sergei LavrovPicha: Reuters

Damu yaendelea kumwagika

Hatua ya kusimamisha mapigano ni sehemu ya mpango wa hatua sita uliofikiwa, kutokana na juhudi za mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya nchi za Kiarabu Kofi Annan juu ya kuutatua mgogoro nchini Syria. Hatua nyingine muhimu katika mpango huo ni kuitaka serikali ya Syria iruhusu misaada kupelekwa kwa wananchi.

Mjumbe maalum wa Syria, Kofi Annan
Mjumbe maalum wa Syria, Kofi AnnanPicha: Reuters

Lakini pana mashaka iwapo serikali ya Syria na wapinzani watautekeleza kikamilifu mpango huo. "Damu inaendelea kumwagika. Kila siku tunapata taarifa juu ya wahanga na juu ya mashambulio," alisema Annan. "Mashambulio yanayofanywa na wanajeshi kwenye makaazi ya raia bado yanaendelea. Na kwa upande wake serikali ya Syria inalalamika juu ya mashamabulio yanayofanywa na watu wenye silaha dhidi ya askari na raia. Mali za watu pia zinashambuliwa."

Annan kutuma barua kwa baraza la usalama

Hali hiyo iliyoelezewa na Mjumbe maalamu wa Syria, Kofi Annan ilijiri hadi kufikia muda wa kuanza kusimamisha mapambano nchini Syria.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki MoonPicha: Reuters

Mpango wa Kofi Annan unazingatiwa kuwa fursa ya mwisho ya kuutatua mgogoro nchini humo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon anahofia madhara yanayoweza kutokea ikiwa pendekezo la Annan halitatekelzwa. Ameeleza: "Wengi wameuelezea mpango wa Annan kuwa ni fursa ya mwisho ya kuutatua mgogoro wa nchini Syria kwa njia ya amani. Baadhi wanahofia kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe ikiwa diplomasia itashindikana."

Annan ameeleza kwamba leo atatuma barua kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufuatia kuisha kwa muda uliowekwa wa kuondoa wapiganaji.

Mwandishi: Leidholdt Ulrich

Tafsiri: Mtullya Abdu/Elizabeth Shoo

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman