1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muafaka washindikana Ugiriki

Admin.WagnerD9 Februari 2012

Mazungumzo ya wanasiasa nchini Ugiriki yamemalizika bila muafaka juu ya mageuzi na hatua za kubana matumizi, ambavyo viliwekwa na wakopeshaji kama sharti la kupewa mkopo mpya wa kuinusuru nchi hiyo usifirisike.

https://p.dw.com/p/1401U
Wakuu wa vyama nchini Ugiriki wameshindwa kupata muafaka juu ya hatua za kubana matumizi.
Wakuu wa vyama nchini Ugiriki wameshindwa kupata muafaka juu ya hatua za kubana matumizi.Picha: Reuters

Baada ya mazungumzo ya wanasiasa kushindwa kupata makubaliano kamili, Waziri wa Fedha wa Ugiriki Evangelos Venezilos amefunga safari kwenda Brussels kukutana na wafadhili, huku akibeba mkataba usiokamilika.

Pande tatu zilizokubali kuipa Ugiriki mkopo wa kuukwamua uchumi wake, yaani Umoja wa Ulaya, Shirika la Fedha Ulimwenguni, IMF, na Benki Kuu ya Ulaya zimeghadhabishwa na kushindwa kwa vyama vikuu vya Ugiriki kufikia makubaliano juu ya masharti yaliyowekwa na pande hizo, kabla ya kuipatia nchi hiyo mkopo mwingine wa euro bilioni 130 ambao inauhitaji kwa dharura kabla ya tarehe 20 mwezi Machi.

Waziri wa Fedha wa Ugiriki Evangelos Venizelos
Waziri wa Fedha wa Ugiriki Evangelos VenizelosPicha: dapd

Maafisa wa kanda inayotumia sarafu ya Euro wanasema makubaliano hayo lazima yafikiwe, na pia yakubaliwe na wakopeshaji kabla ya tarehe 15 Februari, ili utaratibu wa kuutoa mkopo huo uanze kwa muda unaofaa kuepusha mtafaruku kwenye uchumi wa dunia.

Hata hivyo baada ya mazungumzo ya usiku kucha kati ya viongozi wa Ugiriki na wakaguzi kutoka upande wa wakopeshaji, Waziri wa Fedha wa nchi hiyo Evangelos Venezilos aliibuka muda mfupi kabla ya mapambazuko, na kutangaza kwamba muafaka umekwama juu ya kipengele kimoja.

Alisema anaondoka kwenda Brussels akiwa na matumaini kwamba mkutano wa Umoja wa Ulaya utafanyika, na kwamba maamuzi mema juu ya mpango wa kutoa mkopo mwingine yatafikiwa. Alisema kuwa mustakabari wa uchumi wa Ugiriki unategemea mpango huo, na hivyo ni jukumu la kila upande kuwajibika.

Lakini kwa maoni ya Otto Fricke, kutoka Kamati ya Bajeti katika Bunge la Ujerumani, maamuzi yanayofanywa nchini Ugiriki yana mtizamo wa kisiasa.

''Tunapaswa kutambua kwamba baadhi ya wanaojadiliana wanachukua maamuzi wakizingatia uchaguzi unaofuata. Na hiyo ndio maana pengine wanasema kitu hiki lakini wanafanya kingine. Hilo ndilo linaloua matumaini yetu. Tumesema tangu mwanzo kwamba kungekuwepo wataalamu ambao wangetueleza ni vigezo gani vimetekelezwa, na vipi vimeshindikana.'' Alisema Fricke.

Kwa mujibu wa msemaji wa chama cha PASOK ambacho kimeshiriki katika mazungumzo, suala la malipo ya uzeeni ndilo limekuwa kizingiti kikubwa kwenye muafaka uliotarajiwa. Afisa mmoja wa ngazi za juu serikalini amesema wamekubaliana juu ya asilimia 90 ya makato yaliyopendekezwa, na kwamba pengo dogo linasalia kwenye mahesabu.

Ugiriki inakabiliwa na mgogoro mkubwa kiuchumi
Ugiriki inakabiliwa na mgogoro mkubwa kiuchumiPicha: Reuters

Magazeti nchini Ugiriki yamepinga kile yalichokiita ukatiri uliomo kwenye masharti ya wakopeshaji, lakini kwa kukata tamaa yakaonya kwamba hakuna chaguo jingine bali kukubali na kusaini makubaliano.

Ugiriki imekuwa ikizama katika mgogoro mwingine wa kiuchumi tangu kupokea mkopo wa kwanza mwaka 2010. Asilimia 18 ya watu wanaoweza kufanya kazi nchini humo kwa sasa hawana ajira.

Mpango mpya ambao kwa sasa unajadiliwa, unajumuisha mkopo mpya wa euro bilioni 130 kutoka pande tatu za wakopeshaji, na kusamehewa baadhi ya madeni na taasisi za kifedha, lengo likiwa kupunguza mzigo wa madeni unaoilemea nchi hiyo ya kanda ya euro na kunusuru uchumi wake usifirisike kabisa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef