1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Msukumo mpya kwa mzozo wa Darfur

Marekani,China na matafa mengine 15 leo hii yanafunguwa mkutano mjini Paris kuimarisha juhudi za kimataifa kukomesha umwagaji damu katika jimbo la Dafur nchini Sudan.

Wakimbizi wa Darfur wana mustakabali gani?

Wakimbizi wa Darfur wana mustakabali gani?

Lakini Sudan yenyewe haihudhurii mkutano huo wa siku mmoja unaofanyika baada ya Rais Omar Hassan al Bashir kukubali uwekaji wa kikosi mchanganyiko cha Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kulinda amani Dafur.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleeza Rice ambaye amekutana na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa kabla ya mkutano huo amesema ni muhimu kwa serikali ya Sudan kutimiza ahadi yake ya kuruhusu wanajeshi 20,000 wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa huko Dafur.

Kikosi hicho mchanganyiko kitaimarisha kwa kiasi kikubwa kikosi cha wanajeshi 7,000 wa Umoja wa Afrika chenye zana dhaifu kiliopo hivi sasa huko Dafur ambacho kimeshindwa kukomesha umwagaji damu huko Dafur tokea kuwekwa kwao hapo mwaka 2004.

Rice anaona jumuiya ya kimataifa imeshindwa kutimiza wajibu wake katika suala la Dafur.

Amesema mafanikio ya mkutano huo yatategemea nia ya kuisisitiza serikali ya Sudan kuruhusu kikosi hicho cha Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kuingilia kati hali ya Dafur.

Vita katika jimbo hilo la Dafur ni kati ya waasi na serikali ya Sudan inayohodhiwa na Waarabu na kuungwa mkono na wanamgambo wa Janjaweed ambao kiongozi wao anashutumiwa kwa uhalifu wa vita.

Marekani imeulezea umwagaji damu wa Dafur kuwa mauaji ya halaiki na imechukuwa hatua ya kuimarisha vikwazo dhidi ya Sudan licha ya upinzani kutoka China mteja mkubwa wa mafuta wa serikali ya Sudan na ambayo huiuzia serikali hiyo silaha kwa wingi.

Matumaini ya kuendeleza mchakato wa amani wa Dafur yamezidi kuwa makubwa wakati China ilipokubali kushiriki kwenye mkutano huo na kuashiria azma mpya kwa upande wa serikali ya China kutumia ushawishi wake kwa Sudan.

Salim Himid waziri wa zamani wa mambo ya nje wa visiwa vya Comoro ambaye anaishi uhamishoni mjini Paris Ufaransa anakubali kwamba China ina dhima muhimu kwenye mkutano huo.

(O-TON Salim)

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na wawakilishi wa Uingereza,Misri,Japani na Urusi pamoja na maafisa kutoka Umoja wa Waarabu na Umoja wa Ulaya wanashiriki kwenye mkuatno huo.

Lakini Umoja wa Afrika ambao ulisimamia na kufanikisha mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Sudan na waasi haushiriki kwenye mkutano huo ambao inauona kama ni kujirudia kwa jitihada zake au kutekwa nyara kwa agenda yake.

(O-TON Salim)

Rais Sarkozy na waziri wake wa mambo ya nje Bernard Kouchner wamelipa suala la Dafur kipau mbele kutokana na wasi wasi wa kuenea kukosekana kwa utulivu katika nchi jirani za Chad na Afrika ya Kati ambazo ni washirika wa Ufaransa katika eneo hilo.

Ufaransa mapema mwezi huu ilianzisha kusafirisha msaada kwa wahanga wa Dafur kwa njia ya anga huko mashariki mwa Chad na inafikiria kutuma kikosi cha kibinaadamu kusaidia wananchi wa Chad 500,000 waliopoteza makaazi yao ndani ya nchi na wakimbizi kutoka Dafur walioko kwenye makambi mashariki mwa Chad.

Hapo jana waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa ametangaza malengo matatu ya mkutano huo ambayo ni kukiunga mkono kikosi kipya cha amani kwa Dafur ambacho amesema yumkini kikaleta tija katika kukomesha mauaji na kuongeza shinikizo la kuanzisha tena mazungumzo ya amani chini ya kivuli cha Umoja wa Afrika na kutowa msaada wa kifedha kwa kikosi cha Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.

Takriban watu 200,000 wameuwawa na wengine milioni mbili na nusu kupotezewa makaazi yao tokea mwezi wa Februari mwaka 2003 ingawa Sudan inasema takwimu hizo zimeongezwa chumvi.

 • Tarehe 25.06.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CB3K
 • Tarehe 25.06.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CB3K

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com