1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msimamo wa Marekani kuhusu Pakistan

P.Martin27 Agosti 2007

Rais wa Pakistan Pervez Musharraf alie mshirika wa Marekani inayoongoza vita dhidi ya ugaidi, anashuhudia umaarufu wake ukipinguka baada ya kutofanikiwa kumfukuza kazi jaji mkuu wa nchi na machafuko yakizuka sehemu mbali mbali nchini humo.

https://p.dw.com/p/CH94
Rais Pervez Musharraf akihotubia mkutano wa amani wa pamoja katika mji mkuu wa Afghanistan,Kabul mapema mwezi wa Agosti
Rais Pervez Musharraf akihotubia mkutano wa amani wa pamoja katika mji mkuu wa Afghanistan,Kabul mapema mwezi wa AgostiPicha: AP

Licha ya kuwa Marekani yaendelea kumuunga mkono Musharraf,yadhihirika kuwa Washington inajitayarisha pia kwa uwezekano wa kiongozi huyo kulazimika kungatuka au kugawana madaraka ya kuiongoza Pakistan.

Ingawa wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema, Washington haimtelekezi Musharraf kwa njia yo yote ile,ni dhahiri kuwa kupunguka kwa umashuhuri wa Jemadari Musharraf pamoja na sauti zinazozidi kupazwa kudai udemokrasia nchini Pakistan,ni mambo yaliyoifanya Marekani kufikiria njia zingine.

Hivi karibuni,mwanadiplomasia mmoja alisema, Washington imemuhimiza Musharraf kutafuta njia zingine za kushirikiana kisiasa na waziri mkuu wa zamani wa Pakistan,Benazir Bhutto.Yaonekana kuwa azma ya juhudi hizo,ni kumuimarisha Musharraf nyumbani na kuhakikisha kuwa Pakistan itaendelea kushirikiana na Marekani,kupiga vita ugaidi.

Mkakati huo lakini una hatari zake,kwani Washington inaweza kulaumiwa kuwa inaingilia kati mambo ya ndani ya Pakistan;na Bhutto nae huenda akajitia doa kwa kushirikiana na Jemadari Musharraf alieingia madarakani kwa njia ya mapinduzi bila ya kumwaga damu.

Isitoshe,juma lililopita,Mahakama Kuu ya Pakistan iliamua kumruhusu waziri mkuu mwingine wa zamani, Nawaz Sharif,kurejea nyumbani baada ya kuwa uhamishoni kwa miaka saba.Sharif alipinduliwa na jeshi la Pakistan,baada ya kiongozi huyo wa zamani kujaribu kumuondosha Musharraf kama mkuu wa majeshi,jemadari huyo alipokuwa nje ya nchi.

Kwa maoni ya wachambuzi,ikiwa Sharif atarejea nyumbani basi Musharraf atakabiliana na shinikizo kubwa ndani ya nchi.Ni matumaini ya Musharraf kuwa atashinda uchaguzi unaotazamiwa kufanywa majira ya mapukutiko na hivyo kuendelea kama rais kwa awamu ya pili.Chaguzi za bunge zinatazamiwa kufanywa baada ya uchaguzi huo wa rais.

Lakini afisa wa ngazi ya juu katika serikali ya Marekani,amekanusha kuwa Washington inajaribu kujitenga na Musharraf,ambae kufuatia mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001,aliamua kuiunga mkono Marekani,kuiangusha serikali ya Taliban nchini Afghanistan iliyokuwa ikitoa hifadhi kwa wanachama wa Al-Qaeda.