1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msemaji wa kiongozi wa Libya asema Gaddafi bado yupo nchini

7 Septemba 2011

Msemaji wa kiongozi wa Libya Muammar Gadafi amenukuliwa leo akisema kuwa kiongozi huyo hajatoroka kutoka nchini humo.

https://p.dw.com/p/12UHT
Muammar Gaddafi bado yupo nchini Libya.Picha: picture-alliance/dpa

Matamshi hayo yanawadia siku moja baada ya msafara wa magari ya Libya kuonekana kuvuka mapaka na kuingia katika nchi jirani ya Niger. Caro Robi na maelezo zaidi.

Msemaji Moussa Ibrahim alikiambia kituo cha televisheni kilicho Syria Al Rai kuwa kiongozi huyo wa Libya bado yuko nchini humo,ana afya njema na yuko katika hali shwari,licha ya uvumi wa hapo jana kuwa huenda masafara huo wa magari ulikuwa ukimsafirisha Gadafi.

Bürgerkrieg in Libyen Erfolg der Rebellen
Msemaji wa kiongozi wa Libya Moussa IbrahimPicha: dapd

Ibrahim alisema kiongozi huyo hataweza kufikiwa na waasi na kuongeza kuwa mwanawe wa kiume Saif al Islam pia bado yuko nchini humo akisafiri kutoka eneo moja hadi jingine.

Kufikia sasa hakuna ajuaye aliko Gaddafi lakini mshirikishi wa juhudi za kumsaka kiongozi huyo Hisham Buhagiar aliliambia shirika la habari la Reuters na Ufaransa kuwa mara ya mwisho wakimfuatilia alionekana akielekea mpaka wa kusini mwa Libya na kwamba magaai yaliyokuwa yakibeba wanajeshi wa Gaddafi yalivuka kuelekea Niger.

Buhagiar alisema ripoti zinadokeza kuwa huenda akawa katika eneo la kusini mwa kijiji cha Ghwat yapata kilomita 300 kaskazini mwa mpaka na Niger siku tatu zilizopita.

Alisema anadhani kuwa ameshatoka katika kijiji cha Bani Walid kwani watu waliona magari yakielekea katika kijiji cha Ghwat na kwamba huenda anaelekea nchini Chad au Niger.

Duru za kijeshi za Ufaransa na Niger zimedokeza kuwa msafara wa karibu magari 250 ulisindikizwa kuelekea mji wa kaskazini wa Agadez na majeshi ya Niger ambao kulingana na Ufaransa huenda msafara huo ukamjumuisha Gadafi akiwa njiani kuelekea Burkina Faso ambayo ilikuwa imejitolea kumpa hifadhi.

Marekani imesema inaamini kuwa msafara huo ulikuwa umebeba viongozi wa ngazi za juu wa Gaddafi na kuitaka Niger kumzuia yeyote ambaye anatakikana kwa mashataka ya uhalifu wa kivita wakati wa ghasia dhidi Gaddafi nchini Libya.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Leon Panetta alisema Gaddafi ni mtoro lakini Marekani haina sababu ya kuamini kuwa kiongozi huyo ameondoka Libya jambo ambao lilithibithishwa na msemaji wa kiongozi huyo.

Leon Panetta Verteidigungsminister USA NO FLASH
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Leon PanettaPicha: AP

Waasi ambao walimng'oa kiongozi huyo wa muda mrefu madarakani wikii mbili zilizopita pia wanafikiri magari kadhaa yaliyovuka mpaka huenda yalikuwa yamebeba fedha na dhahabu zinazoaminika kuporwa kutoka tawi moja la benki kuu lililoko katika mji alikozaliwa kiongozi huyo.

Ufaransa,Niger,Burkina Faso,waasi pamoja na jumuiya ya Nato wote wamekanusha kujua aliko Gaddafi au kuafikiwa mapatano yoyote ya kumruhusu atoke Libya kutafuata hifadhi kwa raia wa Libya walio katika mataifa mengine ama kwa mahakama ya kimataifa ya kushughulikia kesi za uhalifu ICC inayomtaka kwa mashataka ya uhalifu wa kivita.

Waziri wa mambo ya ndani wa Niger Abdou Labo aliuambia mkutano wa waandishi habari kuwa hakujua kuhusu msafara wa magari kuingia nchini humo lakini akathibitisha kuwa mkuu wa usalama wa Gaddafi aliruhusiwa kuingia Niger kwa misingi ya kibinaadamu na kwamba ndiye afisa pekee wa Libya aliyeruhusiwa.

Mwandishi: Caro Robi

Mhariri: Othman Miraji