1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msako wa taifa zima Ujerumani

9 Oktoba 2016

Polisi ya Ujerumani Jumapili (09.10.2016) imeendelea na msako wake wa mwanaume wa Syria anayetuhumiwa kupanga shambulio la kijihadi wakati wapelelezi wakimhoji mwenzake baada ya kugunduwa vilipuzi katika nyumba yao.

https://p.dw.com/p/2R3Ps
Deutschland Polizeieinsatz in Chemnitz
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Meyer

Mwanaume anayehojiwa ambae pia ni Msyria aliekamatwa siku moja kabla ametakiwa aendelee kubakia mahabusu na hakimu kwa madai ya kusaidia kupanga shambulio baya la matumizi ya nguvu.

Usalama umeimarishwa katika viwanja vya ndege na vituo vya treni kwa vile haijulikani iwapo mwanaume huyo anayesakwa Jaber Albakr mwenye umri wa miaka 22 alikuwa amebeba vitu vya kutengenezea mabomu au silaha.

Polisi imesema kupitia mtandao wa Twitter kwamba "Msako wa mtuhumiwa huyo unaendelea na hatujuwi mahala alipo na amemeba kitu gani.Muwe waangalifu."

Albakr aliwakwepa makomandoo chupu chupu alfajiri ya Jumamosi wakati walipokuwa wakijiandaa kumkamata katika nyumba yake kwenye mji wa mashariki wa Chemnitz nchini Ujerumani ulioko kama kilomita 260 kusini mwa mji mkuu wa Berlin.

Gazeti la kila wiki la Spiegel limeripoti kwamba polisi ilifyetuwa risasi ya kutowa onyo wakati ilipomuona mwanaume mmoja akiondoka kwenye jengo la enzi ya utawala wa Kikomunisti Ujerumani ya Mashariki lakini alifanikiwa kutoroka na kutaja kitendo hicho kuwa kinawezekana kuwa kuboroga kwa polisi.

Vilipuzi hatari vyagunduliwa

Deutschland Polizeieinsatz in Chemnitz nach Sprengsatzfund
Mji wa Chemnitz karibu na nyumba kulikokutikana vilipuzi,Picha: DW/N. Conrad

Polisi imesema imegunduwa gramu kadhaa za baruti ambazo ni hatari kuliko hata TNT katika nyumba na kwamba hata ingelikuwa ya kiwango kidogo ingeliweza kusababisha uharibifu mkubwa sana.

Vyombo vya habari vya ndani ya nchi vimeripoti kwamba vitu hivyo ambavyo kikosi cha kuteguwa mabomu imeviangamiza kwa njia ya mripuko uliodhibitiwa ni bomu lililotengenezwa kienyeji (TATP) linajulikana kama "mama wa shetani " ambalo lilitumiwa na wapiganaji wa jihadi katika mashambulizi ya Paris na Brussels.

Duru za polisi zimeliambia shirika la habari la AFP hapo Jumamosi kwamba Albakr yumini akawa na dhamira za Waislamu wa itikadi kali.Shirika la habari la Ujerumani dpa likitaja duru za usalama limesema inaaminika kwamba alikuwa na mahusiano na kundi linalojiita Dola la Kiislamu.

Mtuhumiwa alikuwa mhamiaji

Fahndung nach Syrer Dschaber Al-Bakr nach Sprengstoff-Fund in Chemnitz
Huyu ndie mtuhumiwa anayesakwa Al-Bakr.Picha: picture-alliance/dpa/Polizei Sachsen

Polisi imewatia mbaroni washirika watatu wa Albakr wanaojulikana hapo Jumamosi wakati wakiwachilia wawili mmoja ameendelea kushikiliwa.

Msemaji wa polisi Tom Berhardt amesema miongoni mwa waliokamatwa hapo Jumamosi katika kituo cha reli cha Chemnitz ni mtu aliyekodi nyumba ambayo imepekuliwa hapo Jumamosi na kugundulikana kwa gramu mia kadhaa za vilipuzi.

Amesema uchunguzi juu ya ushiriki wa mtu huyo unaendelea na amefikishwa kwa hakimu ili aendelee kubakia mahabusu.Ameongeza kuwa msako wa Albakr umepanuliwa hadi nje ya mipaka ya Ujerumani ambapo polisi imekuwa na mawasiliano na wenzao katika nchi nyengine za Umoja wa Ulaya.

Gazeti la Spiegel limesema Albakr alikuwa ameingia Ujerumani hapo tarehe 18 mwezi wa Februari mwaka 2015 na wiki mbili baadae aliwasilisha maombi ya kupatiwa hifadhi nchini ambayo yalikubaliwa hapo mwezi wa Juni mwaka jana.

Mwandsihi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Bruce Amani