Msako wa mavazi walaumiwa | Masuala ya Jamii | DW | 30.04.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Msako wa mavazi walaumiwa

Msako wa hivi karibuni dhidi ya mavazi yasiyokubalika nchini Iran umelaumiwa zaidi na wapinzani na wafuasi wa kihafidhina ambao wamekosoa njia zinazotumiwa na polisi katika kutekeleza msako huo chini ya utawala wa serikali ya rais Mahmoud Ahmednejad.

Rais Mahmoud Ahmednejad wa Iran

Rais Mahmoud Ahmednejad wa Iran

Msako huo unachukuliwa kuwa ni kinyume cha ahadi zilizowekwa na rais Mahmoud Ahmednejad za wakati wa uchaguzi.

Utawala nchini Iran umejaribu kujitenga na kuhusishwa kwake na msako huo na msemaji wa serikali amesisitiza mara kwa mara kuwa serikali haihusiki kamwe na msako huo.

Lakini wadadisi wanaonelea kuwa haiwezekani kuwa serikali haihusiki kwani wanadai waziri wa mambo ya ndani ya nchi amekiamuru kikosi cha polisi kitekeleze msako huo na yeye mwenyewe ameuunga mkono mpango huo.

Wapinzani wa serikali ya Tehran kwa muda mrefu wamekuwa wakipiga kelele kuwa serikali inawakandamiza vijana kwa kisingizio eti wanaubeza autawala wa kiislamu kutokana na jinsi wanavyo vaa.

Rais Mahmoud Ahmednejad anawalaumu wapinzani na amewaita kuwa ni maadui wa serikali yake ambao wanawahimiza vijana wayakiuke maadili ya kiislamu kuhusiana na mavazi na pindi Jamuhuri hiyo ya Kiislamu inapofanya msako dhidi vijana hao basi nao wanajenga chuki dhidi ya serikali.

Rais Ahmednejad amesema kwamba vijana nchini mwake wanatumiwa na maadui kuharibu sifa nzuri ya utawala wa kiisalmu.

Kwa kawaida msako dhidi ya mavazi yasiyofaa hufanyika wakati wa kiangazi ambapo jua huwa ni kali mno na joto kuzidi kiwango, hali hiyo huwafanya wanawake na hasa wasichana kuvaa mavazi ambayo yanakiuka sheria kali ya mavazi ya Iran, na hapo serikali huwajibika kuingilia kati.

Polisi katika barabara za mji mkuu wa Tehran huonekana wakiwasimamisha wasichana na kuwaamuru wafunike vichwa vyao au hata kufuta vipodozi walivyojipaka usoni.

Mavazi ya kubana, suruali fupi za kupwaya au hata makubadhi yanayo onyesha miguu ya mwanamke hayo yote ni matendo yanayohalifu sheria nchini Iran na unaweza kuwekwa kizuizini.

Polisi nchini Iran huwasimamisha pia wanaume mara kwa mara kwa kile wanachokiita sura zisizo ridhisha au hata wanapopiga muziki kwa sauti ya juu ndani ya magari yao.

Sura zisizo ridhisha kwa wanaume ni pale mwanamume anapokata nywele zake kwa mitindo ya kisasa au hata ndevu zake kujifananisha na waonyesha mitindo wa nchi za magharibi na kwa upande wa mavazi ni pale anapo valia mashati yaliyokatwa mikono au pia T- sheti zenye maandishi yanayodhaniwa kuwa hayafai.

Lakini wakati huu hali ni tofauti kabisa, utawala wa Tehran unavuka mipaka kwa kile wanacho kiita kuokoa maadili mema hicho ni kilio cha wapinzani nchini Iran.

Maelfu ya vijana wa kike na wakiume wameonywa katika barabara za jijini Tehran na wale waliofikia hatua ya kupelekwa katika vituo vya polisi basi hupigwa picha za kumbukumbu kwa mujibu wa kanali wa Mohammad Hosseini wa duru za kisheria nchini Iran.

Kufuatia marufuku iliyowekewa wanafunzi wa chuo kikuu cha Shiraz dhidi ya kuvaa suruali fupi na mashati yasiyo na mikono hata ndani ya mabweni yao wanafunzi hao walifanya mgomo siku ya jumatatu iliyopita na kudai muhadhiri wa chuo hicho ajiuzulu.

Zaidi ya wanafunzi 2000 wa kike na wakiume wa chuo hicho kikuu cha Shiraz walitoa orodha ya malalamiko yao ikiwa ni pamoja na madai ya kutaka vijana wapewe uhuru wa kujiamulia mambo yao ya kibinafsi.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com