1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msako dhidi ya magaidi washika kasi Uengereza na Australia

Oummilkheir3 Julai 2007

Jumla ya watu wanane,wengi wao madaktari watuhumiwa kua nyuma ya njama zilizoshindwa za mashambulio huko London na Glasgow

https://p.dw.com/p/CHBj
Picha: picture-alliance/dpa

Uchunguzi wa njama zilizoshindwa za mashambulio ya mabomu mijini London na Glasgow umeelekezwa Australia hivi sasa ambako mtuhumiwa wanane amekamatwa-na yeye pia ni daktari,mwenye asili ya India lakini.

Tabibu wa pili ambae hakutangazwa ni raia wa nchi gani,anahojiwa na polisi ya Australia,bila ya kuandamwa kisheria.

Mtu ,mwenye umri wa miaka 27 alikamatwa jana usiku katika uwanja wa ndege wa Brisbane,alipokua akitaka kuihama Australia kuelekea mahala kusikojulikana bila ya tikiti ya kurudi.

Kwa mujbiu wa shirika la habari la la Australia AAP,alikua anataka kuelekea India, kupitia Malaysia.

“Amekamatwa na anahojiwa hivi sasa amesema waziri mkuu wa Australia John Howard mbele ya waandishi habari na kuongeza:

“Yote haya yanadhihirisha ushirikiano wa dhati ulioko kati ya maafisa wa idara za usalama za Australia na wenzao wa Uengereza.”

Daktari huyo ambae hakutajwa ni raia wa nchi gani amekua akifanya kazi tangu September mwaka jana katika hospitali ya Gold Coast,karibu na Brisbane ambako wenzake wanamtaja kua “raia mwema na daktari kijana mwenye ujuzi”-kama asemavyo waziri mkuu wa jimbo las Queensland Peter Beattie.Alikua akiishi Liverpool hapo awali kabla ya kupata kazi nchini Australia.

Daktari wa pili,anaetokea pia Liverpool,na anahojiwa wakati huu tulio nao.”Lakini haijulikani kama anahusika kwa namna yoyote ile na njama iliyoshindwa ya mashambulio ya London.Ameongeza kusema waziri mkuu wa jimbo la Queensland la Australia.

Wasif wa mtu huyu wa nane aliyekamatwa Australia unafanana moja kwa moja na ule wa wanaume sita na mwanamke mmoja waliokamatwa Uengereza.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uengereza,madaktari wasiopungua watano huenda wakawa miongoni mwa watu hao sabaa waliokamatwa tangu jumamosi iliyopita nchini Uengereza.

Mbali na daktari aliyetiwa mbaroni nchini Australia,daktari mwengine ,mpalastina mwenye uraia wa Jordan,Mohammed Jamil Abdelkader Asha,mwenye umri wa miaka 27 amekamatwa pamoja na mkewe,ambae ni mfanyakazi wa maabara,karibu na Liverpool.

Maafisa wa Jordan ambao hawakutaka majina yao yatajwe wanaamini pengine Mohammad Asha ndie muasisi wa njama iliyoshindwa ya mashambulio ya London.

Duru za polisi ya Uengereza zinasema daktari wa pili ni raia wa Irak.Kwa mujibu wa kituo cha matangazo cha BBC,huenda yeye ndie aliyekua nyuma ya njama iliyoshindwa ya mashambulio ya Glasgow.Viongozi wa serikali ya Scottland ,sawa na polisi na wakaazi wa eneo hilo wanaamini waislam wanaoishi katika eneo hilo hawana mafungamano yoyote na njama hizo zilizoshindwa za mashambulio.Osama Saeed wa jumuia ya waislam wa Scottland anasema:

“Tunafurahishwa na matamshi kama hayo.Yanatupa moyo.Sawa na matamshi mengi kama hayo yanayotolewa na Polisi.Waislam wnaweza kuendelea kuishi vyema katika Scottland.Tunaamini jamii inatambua tofauti iliyoko kati ya magaidi kwa upande mmoja na waislam,wakristo,wayahudi na wengineo wasioabudu Mungu kwa upande wa pili.”

Wakati msako dhidi ya magaidi watuhumiwa unaendelea nchini Uengereza na Australia,polisi ya London imetegua kifurushi kilichofichwa karibu na kituo cha usafiri wa chini kwa chini huko Hammersmith-magharibi ya London.

Mashambulio ya kigaidi yamegharimu maisha ya watalii sabaa wa Hispania na wakalimani wao wawili wa kiarabu katika mkoa wa Maarib ,mashariki ya Yemen.Wafuasi wa mtandao wa kigaidi wa Al Qaida wanatuhumiwa kua nyuma ya mashambulio hayo.